Wachezaji 33 wamependekezwa na Kamati ya Ufundi ya Simba SC wasajiliwe kwa ajili ya msimu ujao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema orodha hiyo itawasilishwa Kamati ya Usajili na kujadiliwa ili kupata orodha fupi ya wachezaji wa kusajiliwa.

Hata hivyo, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kabla ya mchakato huo, jioni ya leo watakuwa na kikao na kocha Mganda, Jackson Mayanja kupokea ripoti yake pia.

Amesema Mayanja naye atakuwa na orodha ya wachezaji anaotaka wasajiliwe ambayo italinganishwa na orodha ya Kamati ya Ufundi.

“Tutazijadili pamoja ripoti hizo na kuchukua idadi ya wachezaji ambao wanahitajika kwa mujibu wa mahitaji ya kocha. Suala la nani asajiliwe, tutajadili kwa pamoja, Kamati ya Usajili, Kamati ya Ufundi na benchi la Ufundi,”amesema.

Amesema orodha ya wachezaji 33 iliyowasilishwa na Kamati ya Ufundi inahusisha wachezaji wa kigeni na wazawa, kati yao wakiwemo ambao wamemaliza mikataba na timu za hapa nyumbani.

“Mimi ninawaomba wana Simba wawe na subira tu, zoezi la usajili linafanyika kwa umakini mkubwa sana, na tunaangalia mambo mengi sana, hatutaki kurudia makosa. Hatutaki kusajili tena mamluki,”amesema.

Mambo Yameiva Old Trafford, Mourinho Kutambulishwa Rasmi
PICHA 9 KUTOKA ZAMBIA MKUTANO WA ADB, MAJALIWA AMWAKILISHA JPM