Vinara wa Ligi Kuu Ya Soka Tanzania Bara, Simba wameondoka leo saa 1:00 asubuhi kwenda Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi ambalo  limeanza jana, timu hiyo imetamba kuendeleza wimbi lake la ushindi kama ilivyo katika Ligi Kuu Bara.

Katika ligi kuu, Simba inaongoza ikiwa na pointi 44 ikifuatiwa na Yanga yenye 40 huku Azam FC ikiwa ya tatu na pointi 30.

Simba ipo Kundi A na timu za Taifa Jang’ombe, URA, KVZ, Jang’ombe Boys, inatarajiwa kucheza mechi yake ya kesho Jumapili dhidi ya Taifa Jang’ombe saa 2:30 usiku kwenye Uwanja wa Amaan, wakitanguliwa na mechi kati ya KVZ na URA saa 10:00 jioni uwanjani hapo.

Kabla ya kuondoka mjini Dar es salaam, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema: “Tunataka kuendeleza kasi yetu ya ushindi kwenye michuano hii ya Mapinduzi, hatutazubaa, tutaifunga kila timu.

“Pia tumepanga kuwatumia wachezaji ambao hatuwatumii sana kwenye ligi ili wapate nafasi ya kuboresha viwango vyao.”

Kati ya wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Simba ni Laudit Mavugo, Frederick Blagnon, Hamad Juma, Peter Manyika na Novalty Lufunga.

Mayanja alisema wamepanga kutengeneza mzunguko wa wachezaji katika michuano hiyo na watatoa kipaumbele kwa wachezaji wa benchi.

“Tulichokipanga kama benchi la ufundi ni kuwapa nafasi ya kucheza wachezaji wetu wa akiba ambao hawakutumika sana, tunataka kuona uwezo wao wa ndani ya uwanja baada ya kukosa nafasi ya kucheza.

“Wachezaji hao wa akiba tutawachanganya na wale wa kikosi cha kwanza tuliokuwa tunawatumia kwenye ligi kuu na lengo letu ni kuwapumzisha nyota waliotumika sana katika ligi kuu,” alisema Mayanja.

Serikali yakanusha uhaba wa dawa za usingizi hospital ya bombo mkoani tanga
Gonzalo Higuain Achizika Kwa Paulo Dybala