Watani wa Jadi, Simba na Yanga leo wameshindwa kutambiana ndani ya dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika ‘Derby’ ya Kariakoo iliyovuta umakini wa mamilioni ya washabiki wao nchini.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu inayopewa nguvu na Vodacom imemalizika kwa sare ya 1-1, magoli yaliyofungwa na Amisi Tambwe dakika ya 26 na Shiza Kichuya kwa upande wa Wanamsimbazi akifumania nyavu dakika ya 86.

Kichuya ameifunga Yanga kwa mara ya kwanza, lakini pia goli hilo la kusawazisha liligeuka kuwa dhahabu kwa timu hiyo ambayo ilikuwa ikicheza kwa upungufu baada ya Jonas Mkude kupigwa kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza.

Simba ambao bado hawakubaliani kwa moyo mmoja na goli la Yanga wakidai lilipatikana baada ya Tambwe kunawa mpira na kufanikisha kuwapenya walinzi, wameonekana kuvaa furaha ya mchezo zaidi kutokana na kuwa katika kipindi cha majonzi na sintofahamu tangu dakika ya 27 ya mchezo.

“Ile kadi na goli vilitutoa katika mchezo lakini baada ya kumsikiliza kocha tumeweza kurejea na kupata goli,” alisema Mwinyi Kazimoto baada ya kumalizika kwa mchezo huo. “Ninawaomba mashabiki wa Simba tuendelee kuwa pamoja naimani hili kombe tutalichukua,” aliongeza.

Kutokana na matokeo hayo, Simba imeendelea kujikita kileleni mwa Ligi hiyo kwa kufikisha ‘pointi’ 17 huku Yanga ikifikisha Pointi 11. Vilevile, Simba imeendelea kuweka rekodi yake vizuri kwa kutopoteza pointi 3 tangu msimu huu uanze.

Video: Makamu wa Rais aagiza kampeni ya kupanda miti kuwa endelevu nchi nzima
Video: Wanasheria Ukawa kupambana na Prof. Lipumba