Kikosi cha Simba, kinaondoka hii leo kuelekea mjini Unguja visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya siku nne kabl ya kuwakabili Mwadui FC mwishoni mwa juma hili.

Kikosi cha Simba kinakwenda kisiwani Unguja, huku kikiwa na kumbukumbu mbaya ya kushindwa kufanya vyema katika michezo mitatu iliyopita ambapo miongoni mwa michezo hiyo miwili ni ya ligi kuu na mmoja ni wa michuano ya kombe la FA.

Simba ilishindwa kufurukuta na kujikuta ikitolewa katika hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la shirikisho kwa kufungwana Coastal Union mabao mawili kwa moja na kisha wakapoteza mchezo wa ligi kuu dhidi ya Toto Africans kabla ya kulazimishwa matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Azam FC.

Kutokana na hali hiyo kikosi cha Simba kitahitaji kujitutumua katika mchezo wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Mwadui FC inayofundishwa na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye aliwahi kuwa muajiriwa wa Simba kwa vipindi tofauti.

Kikosi cha wekundu hao kinatarajia kurejea jijini Dar es salaam siku ya  jumamosi tayari kwa mchezo huo utakaochezwa siku ya jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.

Wakati huo huo kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib jana alijiunga na wachezaji wenzake na kuanza mazoezi rasmi, baada ya kupona ugonjwa wa Malaria uliokua unamsumbua kwa siku kadhaa zilizopita.

Meneja kikosi cha Simba, Abbas Gazza amesema Ajib aliungana na wenzake na kufanya nao mazoezi.

“Ndiyo Ajib amerejea, amefanya mazoezi na wenzake,” alisema Abbas.

Mourinho Awasilisha Salamu Za Pongezi Kwa Ranieri
Uchaguzi Wa Young Africans Wapigwa Kalenda

Comments

comments