Mabingwa wa soka Tanzania Bara Wekundu Wa Msimbazi Simba, wamewasili jijini Mbeya tayari kwa mpambano wa Ligi kuu dhidi ya Mbeya City utakaopigwa keshokutwa Jumatano kwenye uwanja wa Sokoine.

Kikosi cha Simba kiliondoka Dar es salaam leo asubuhi kwa usafiri wa anga wakitumia ndege ya shirika la ndege la Tanzania (ATCL), na kilipowasili uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Songwe kilipokelewa na baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kongwe nchini.

Kwa kuonyesha mapenzi na bashasha kwa timu yao, baadhi ya mashabiki na wanachama wa Simba SC wa jijini Mbeya, waliisindikiza timu yao hadi Mbeya mjini kwa ajili ya mapumziko, huku wengi wao wakitumia usafiri Pikipiki (Boda Boda).

Simba watakua jijini Mbeya hadi mwishoni mwa juma hili, ambapo baada ya kucheza na Mbeya city watapapatuana na maafande wa Jeshi La Magereza (Tanzania Prisons) siku ya Jumapili Uwanja wa Sokoine.

Endapo kikosi cha Simba kitafanikiwa kushinda michezo yote miwili ya jijini humo kitaendelea kulisogelea taji la ubingwa Tanzania bara na kulitwaa kwa mara ya tatu mfululizo.

Hata hivyo nahodha na mshambuliaji wa mabingwa hao, John Bocco amesema kuwa watakuwa na kazi ngumu mbele ya Mbeya City, ila watapambana na kupata matokeo.

Bocco amesema wachezaji wapo tayari na wanatambua kwamba utakuwa mchezo mgumu ila wanahitaji kupata pointi tatu.

Mshambuliaji huyo aliyefunga zaidi ya mabao 100 katika michezo ya ligi kuu, pia amewaomba mashabiki wajitokeze kuwapa sapoti kwani malengo yeo ni kuona wanapata pointi tatu.

Jumamosi Simba waliibamiza Mwadui FC mabao matatu kwa sifuri Uwanja wa Taifa Dar es salaam, na kufikisha alama 75 ambazo zinaendelea kuwaweka kileleni mwa msimamo wa lLgi Kuu Tanzania Bara.

Mabao ya Simba katika mchezo dhidi ya Mwadui FC yalifungwa na kiungo Hassan Dilunga dakika ya tisa akimalizia pasi nzuri ya mshambuliaji na nahodha, John Raphael Bocco ambaye pia alifunga bao la tatu, huku beki Augustino Simon akijifunga dakika ya 21, alipokua akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na beki Shomari Kapombe kutoka upande wa kulia.

Hata hivyo jana Jumapili Simba SC walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya African Lyon inayoshiriki Ligi Daraja La kwanza Uwanja wa Uhuru Dar es salaam na kushinda mabao matano kwa sifuri, ikiwa ni muendelezo wa kujiweka vizuri kwa michezo inayofata ya Ligi Kuu hususan ya jijini Mbeya dhidi ya Mbeya City na TZ Prisons.

Katika mchezo huo wa kirafiki mabao ya Simba yalifungwa na kiungo Ibrahim Ajibu (mabao mawili dakika za 25 na 30), mengine Mbrazil Tairone Da Silva dakika ya 28, Muzamil Yassin dakika ya 32 na Mkongo Deo Kanda dakika ya 87.

RPC na Mkuu wa TAKUKURU waponea tundu la sindano fagio la Magufuli Arusha
Shambulizi la kigaidi Uingereza, Mmarekani ni kati ya waliouawa