Simba imeondoka mchana wa leo kwenda Morogoro kwa ajili ya kambi yao ya maandalizi ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City, mechi hiyo itachezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Simba imekwenda mkoani humo ikiwa imeiondoa Singida United kwa mabao 5-1 kwenye michuano ya Kombe la FA na wao kutinga hatua ya robo fainali sawa na Yanga, Ndanda, Mwadui, Prisons na Coastal Union.

Simba inaonekana kuwa na uchu wa kutwaa ubingwa wa VPL ambao pia unawaniwa na Yanga pamoja na Azam ambazo zina pointi 46 kila moja huku Yanga ikiongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa wakati Simba wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa na pointi 45.

Katika mzunguko wa kwanza, Simba iliifunga City kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine jijini Mbeya na sasa imepanga kuendeleza ubabe huo huku City nao wakijipanga vyema kuja kuondoka na pointi tatu na wataingia Dar es Salaam kwa kushitukiza.

Wachezaji wa timu ya Simba wamethibitisha kuondoka jijini na kwamba wanakwenda kujichimbia huko ili kujifua kwani hawataki kupoteza mechi hiyo kama ilivyokuwa mechi iliyopita dhidi ya Yanga ambapo walifungwa bao 2-0 na waliweka kambi mkoani humo.

Sakata La Kashfa Za Jerry Muro, Manara Abisha Hodi Kwa Waziri Nape
Polisi yatolea majibu taarifa za kukamatwa Maalim Seif (Audio)