Mtanzania Alphonce Simbu, amefanikiwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya mbio ndefu za yajulikanayo kama Standard Chartered Mumbai Marathon ya mwaka huu, yaliyofanyika katika jiji la Mumbai nchini India, huku akiwapiku Mkenya Joshua Kipkorir pamoja na wakimbiaji wengine wazoefu kutoka mabara mbalimbali.

 

Mwanariadha huyo ambaye yupo chini ya udhamini wa kampuni ya Multichoice Tanzania, ambao walimfanyia maandalizi mazuri yaliyomletea ushindi baada ya kutumia muda wa saa 2:09:28.

Amesema ushindi huo kwake ni changamoto kwa mashindano mengine makubwa na kwamba huo ni mwanzo tu, na ushindi huo siyo wake peke yake au wadhamini wake , bali ni ushindi wa Taifa zima la Tanzania.

Kwa upande wa Serikali, Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Mh. Nape Nnauye amempongeza kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema , “Tumefanikiwa tena, hongera Simbu, hongera RT (Chama cha Riadha Tanzania), asanteni Multichoice Tanzania kwa kumsapoti. Mungu ibariki Tanzania.”

Mkuu wa Mahusiano wa Multichoice Tanzania Johnson Mshana amesema Multichoice imefurahi sana kwa matokeo huku akisisitiza kuendelea kumdhamini Simbu kwa mujibu wa makubaliano yao, ili kuhakikisha anaendelea kufanya vyema na kuliletea taifa sifa kubwa.

“Tulichukua jukumu la kumdhamini Simbu katika mazoezi na maandalizi yake kwa kipindi cha mwaka mzima, kwani tunafahamu fika kuwa mazoezi na maandalizi ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika mchezo wowote.

Alisema Mshana na kuongeza “Dhamira yetu kubwa ni kuinua vipaji na kulirejesha taifa letu kwenye ramani ya dunia katika ulingo wa michezo na burudani”

Alphonce anatarajiwa kurejea Tanzania Jumatatu hii.

 

Waziri Tizeba awatoa hofu watanzania kuhusu chakula
TPA yashauriwa kurasimisha bandari bubu nchini