Shirikisho la kabumbu nchini Tanzania (TFF) limesema hukumu ya madai ya kughushi saini ya mchezaji Bernard Morrison itatolewa Agosti 10 baada ya kazi ya uchunguzi iliyofanywa na Jeshi la Polisi kumalizika.

Kiungo huyo mshambuliaji kutoka nchini Ghana aliishitaki Young Africans kwa TFF, akidai kuwa saini yake imefaniwa fojari katika mkataba wa miaka miwili, ambao klabu hiyo yenye maskani yake kwenye makutano ta mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam, imeuwasilisha TFF na Shirikisho la kandanda duniani (FIFA).

Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Elias Mwanjala amesema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za uchunguzi wa suala hilo na hawana haja ya kuwa na papara ili kupata majibu sahihi.

Mwanjala amesema awali walipanga kutoa uamuzi wa suala hilo mwishoni mwa mwezi Julai na baadaye kupeleka mwanzoni mwa mwezi huu, lakini walishindwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wao.

Amesema wamewasiliana na Jeshi la polisi na kupata majibu kuwa wanamalizia uchunguzi, na mwishoni mwa juma hili watawasilisha TFF kwa mujibu wa taratibu.

“Siyo suala la kukaa dakika au saa kadhaa na kutoa uamuzi. Jambo hili linahitaji umakini wa hali ya juu ili kupata majibu sahihi. Tumewasiliana na Jeshi la Polisi na kuambiwa kuwa kazi imekwisha na sasa wanaweka sawa taarifa za kiuchunguzi ili kutangazwa na TFF,” amesema Mwanjala.

Kuhusiana na suala la fedha alizopewa Morrison kurejeshwa Young Africans, Mwanjala amesema hakuna taarifa hiyo hadi sasa zaidi ya kusubiri uchunguzi kukamilika.

Mbali na Morrison kuishitaki Young Africans, mabingwa hao wa kihistoria Tanzania Bara pia wamewashtaki mabingwa wa sasa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (ASFC) Simba SC wakidai kuwa wanaingilia mkataba wake na mchezaji huyo kinyume na utaratibu.

“Kwa kifupi masuala yote haya tutayatolea uamuzi wake siku hiyo. Tutakuwa na masuala mengi, ambayo yatatolewa uamuzi, kuna suala la wachezaji kudai mishahara yao, masuala ya mikataba na kesi mbalimbali,” ameongeza ofisa huyo.

Awali, Young Africans walimsajili Morrison kwa mkataba wa miezi sita kwa lengo la kuangalia kiwango chake, na waliporidhishwa kuwa ana uwezo mkubwa kisoka, walidai kumuongezea mkataba wa miaka miwili ambao unamalizika katikati ya 2022.

Young Africans wasema mkataba huo ulisajiliwa TFF na Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) kwa mujibu wa taratibu.

Matola: Azam FC hawajanifuata
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 5, 2020

Comments

comments