Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) imeiondolea adhabu ya kufungiwa kusajili, klabu ya Singida Big Stars.

Uamuzi huo umefanywa na kamati hiyo baada ya kupitia hoja za timu hiyo katika maombi yao ya marejeo (review) kuhusu uamuzi wa awali wa kufungiwa kusajili.

Ikumbukwe kuwa Oktoba 7, 2022 kamati hiyo ya TFF iliifungia Singida Big Stars na Tanzania Prisons kusajili kwa Dirisha moja la usajili baada ya kufanya kosa la kusajili wachezaji wenye mikataba na klabu zingine.

Ambapo Singida Big Stars ilimsajili Kipa Metacha Mnata huku akiwa na mkataba na klabu ya Polisi Tanzania huku Prisons ikimsajili kipa Mussa Mbisa aliyekuwa na mkataba na Coastal Union ya Tanga.

Badala ya kuondolewa kifungo hicho, Singida Big Stars imepigwa faini ya Sh 1 milioni ambayo inatakiwa kulipwa kabla ya dirisha dogo la usajili linalofunguliwa Desemba 15.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari ambayo imetolewa na kamati hiyo imesema iwapo Singida Big Stars haitalipa faini hiyo ndani ya muda uliowekwa, adhabu ya kufungiwa kusajili itabaki palepale.

Ahmed Ally: Ihefu FC imetufurahisha sana
Uharibifu Ukraine: Urusi yakalia kuti kavu