Jeshi la Singida Big Stars limeweka kambi mkoani Dodoma kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Mbeya City unaotarajiwa kupigwa kati ya Machi 30 hadi Aprili 2 kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida.

Mratibu wa Singida Big Stars, Ibrahim Mohammed amesema maandalizi ya kikosi chao yanaendelea vizuri na wanatarajia kupata matokeo mazuri katika mchezo huo, ili wavuke na kutinga Nusu Fainali.

Ibrahim amesema mazingira ya mkoa wa Dodoma pamoja na hali ya hewa yanashabihiana na mkoani Singida, hivyo wameshawishika kuweka kambi mkoani hapo, na siku chache kabla ya mchezo watarejea nyumbani kuisubiri Mbeya City.

“Tumeweka kambi mkoani Dodoma kwa sababu hali ya hewa ya hapa ni sawa na ya Singida kwahiyo tulitaka kubadilisha mazingira kwa wachezaji ili warudishe ule utimamu na morali baada ya kutoka mapumziko ya siku saba.

“Tutakuwa hapa kwa takriban siku nane kisha tutarudi Singida tukiwasubiri Mbeya City na naamini kuwa tutafanikiwa kutinga hatua ya Nusu Fainali kwenye michuano hii.”

“Mazoezini tutawakosa Meddie Kagere pamoja na Yusuph Kagoma ambao wapo kwenye majukumu ya timu ya taifa lakini pia kwenye mechi husika tutamkosa Kelvin Nashon ambaye alipata majeraha mazoezini pamoja na Said Ndemla ambaye ana kadi tatu za njano.” Amesema Ibrahim

Dunia ishikamane mapambano dhidi ya Kifua Kikuu
Kocha Coastal Union matumaini kibao safari ya Dodoma