Uongozi wa Klabu ya Singida Big Stars umekanusha taarifa za kufanya mazungumzo ya awali na Uongozi wa Klabu ya Young Africans kuhusu usajili wa Kiungo kutoka nchini Brazil Bruno Gomez Baroso.

Kwa mujibu wa Gazeti la Mwanaspoti la leo Jumatano (Machi 15), imeelezwa kuwa tayari klabu ya Young Africans imekamilisha sehemu ya usajili wa kiungo huyo, ambaye imeelezwa ana asilimia kubwa ya kuonekana akivaa jezi za rangi ya Njano na Kijani msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa.

Kutokana na taarifa hiyo Dar24 Media tumeona kuna haja ya kupata uhakika kutoka kwa viongozi wa Singida Big Stars ambao kisheria ndio wanamiliki Kiungo huyo ambaye alisajiliwa klabuni hapo mwanzoni mwa msimu huu akitokea nchini kwao Brazil.

Kwa niaba ya Uongozi wa klabu hiyo ya mkoani Singida, tumezungumza na Afisa Habari wa Singida Big Stars Hussein Masanza ili kufahamu kwa kina kinachoendelea katika Biashara ambayo kwa mujibu wa gazeti la Mwanaspoti inadaiwa kufanyika kwa asilimia kadhaa.

Masanza amesema taarifa hizi sio za kweli na huenda zimetolewa kwa makusudi ili kuvuruga mipango ya kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ambao watakutana na Young Africans katika Uwanja wa Liti mkoani Singida mwezi ujao.

“Tumeziona hizo taarifa lakini nikuhakikishie hakuna ukweli wowote kuhusu kufanywa kwa Biashara ya usajili wa Bruno Gomez, huyu ni mchezaji wetu halali na amesaini mkataba wa muda mrefu wa Singida Big Stars.”

“Imekuwa kawaida kwa wachezaji wetu kuhusishwa na taarifa za kuwaniwa na klabu nyingine za hapa Tanzania, hii inatuaminisha kuwa tuna kikosi bora kinachoundwa na wachezaji wenye uwezo wa kucheza popote.” Amesema Masanza

Hata hivyo Dar24 Media tuliwahi kuzungumza na Bruno Gomez na kumuuliza kuhusu taarifa za kuwaniwa na Young Africans na alichotujibu ni kwamba alifika Tanzania kwa ajili ya kucheza soka katika klabu ya Singida ambayo alisisitiza ana malengo nayo makubwa.

Rais Samia awasili Jijini Pretoria kwa ziara ya kikazi
Malezi yazingatie maadili ya mtanzania