Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amesema anachukizwa na suala la urasimu linalochagizwa na rushwa, ukandamizaji wa haki kwa wanyonge na kwamba anaongea akiwa hamuogopi kijana yeyote kwani akivurugwa basi naye atawavuruga watu kwa kiwango cha juu.

Chalamila ameyasema hayo wakati akizungumza na Shirikisho la Umoja wa Wamachinga, Mama Lishe/Baba Lishe, Jamii Mpya, Wanawake Wafanyabiashara, Jukwaa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi na Shujaa wa Maendeleo wa Mkoa wa Kagera na kuongeza kuwa jamii inapaswa kubadilika na kujipanga ili kuondoa urasimu.

Amesema, “Huwa nasikitika sana kwenye suala la urasimu na rushwa hasa wakati wa utoaji wa haki unakuta akina mama na vijana wameunda vikundi vyao lakini hata wakiwa na usajili bado wanayumbishwa na hawapati chochote, sasa naongoea siogopi kijana yeyote mimi nikivurugwa huwa nawavuruga watu kwelikweli, mjipange.”

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila akizungumza na Shirikisho la Umoja wa Wamachinga, Mama Lishe/Baba Lishe, Jamii Mpya, Wanawake Wafanyabiashara, Jukwaa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi na Shujaa wa Maendeleo wa Mkoa wa Kagera.

Chakamila ameongeza kuwa, wapo watu ambao huwaonea wananchi kwa kuwanyang’anya ardhi kwa kuwahonga viongozi wa juu pesa kitu ambacho hukandamiza haki ya wanyonge n kwamba upo umuhimu wa kuwa na viongozi bora watakaobeba maono ya rais kwa kuwahudumua wananchi kwa haki.

“Kuna kipindi niliambiwa hapa masoko hayafunguliwi hadi sijui saa ngapi eti kwa ajili watu wanafanya usafi, mimi nasema masoko yasifungwe na usafi ufanyike wakati biashara zinaendelea huu ni muda wa kukimbizana na uchumi fungua duka uza usafi sio jumamosi tu usafi iwe ni zoezi la kila siku,” amebainisha Mkuu huyo wa Mkoa.

Hata hivyo, Chalamila ameongeza baadhi ya Viongozi wanashindwa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, kwani fedha nyingi zinazoletwa kwa ajili ya maendeleo hurudishwa Serikalini kwa kushindwa kuzielekeza maeneo husika kutokana na mvutano wa wanasiasa usio na tija.

Wakimbizi nchi ya tatu waanza maisha mapya Ughaibuni
EAC yazungumzia mchakato wa amani DRC