Wiki iliyopita nilikupa siri tano za kufanikiwa na nikakuahidi kuwa nitamalizia siri nyingine tano baada ya muda mfupi. Leo nitaendelea kukupa siri hizo ambazo zimegeuka kuwa kikwazo cha mafanikio kwa wengi wasiozifuata.

Kwa kuwa makala ya kwanza iliishia namba tano ya siri hizo, leo nitaanza na namba 6 hadi 10 zinazojikita zaidi katika maisha ya wote. Hivyo, naamini zitakufungua ama kukuongezea kitu kwenye kile unachokijua au kukumbusha zaidi.

  1. Jifunze Bila Kikomo

Kujifunza ni siri kubwa ya mafanikio. Ukiwa na uelewa mkubwa wa jambo fulani unayo nafasi kubwa zaidi ya kulifanikisha. Hakikisha unajifunza jambo jipya karibu kila siku kuhusu kitu unachotaka kukifanya au unachokifanya.

Unaweza kusoma vitabu, mtandaoni, angalia wenzako wanavyofanya au hata kwa kutumia ‘YouTube Tutorial’. Waangalie vizuri marafiki zako na watu unaokutana nao, hakikisha unajifunza kitu kutoka kwao kama wao wanauzoefu zaidi yako. Hata kama hawana uzoefu zaidi yako, wadadisi kufahamu wanafikiria nini kuhusu kitu unachofanya au unachotaka kufanya. Kumbuka ‘ni heri kujifunza kuliko kujua kila kitu’.

Maisha yako ya kila siku pia ni fundisho kwako kwa yale unayoyapitia, hakikisha unajifunza kweli na unayafanyia kazi. Shiriki Semina na makongamano yanayohusu mambo unayotaka kufanya au unayofanya. Fanya mijadala na watu walio kwenye  Nyanja/field hiyo. Usijifungie ndani na kufanya unachokijua. Mwisho, mfundishe mwenzako anayetaka kujifunza kwa kuwa wakati unamfundisha na wewe unaongeza uelewa zaidi.

  1. Tunza Muda/Wakati na Fedha

Muda ni kitu muhimu sana kwa kuwa ndiyo rasilimali pekee ambayo ikiondoka huwezi kuirudisha au kuifidia. Hivyo hakikisha unafanya mambo yako kwa kufuata ratiba nzuri uliyojipangia.

Kuna msemo unasema ‘Muda ni Fedha’ (Time is money)’, tunza vitu hivi viwili kwa umakini sana. Kumbuka watu wote duniani walioendelea walikuwa na tabia ya ‘kusave’ fedha na muda. Hakikisha unajiwekea malengo yako na unakuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha. Jiwekee malengo kwa uhakika, weka akiba ya fedha unayopata na iheshimu sana hiyo akiba.

 

  1. Usiishi Kwa Mazoea

Kama unataka kuendelea, vunja mazoea. Ishi kwa kanuni na taratibu za maisha kulingana na kile unachotaka kukifanikisha. Unapotaka kufanya jambo fulani, mazoea huwa ni kikwazo kikubwa sana bila wewe kufahamu na ndio maana unashauriwa sana kufikiria nje ya sanduku ili ufanye kitu cha kipekee.

 

  1. Geuza Matatizo/Changamoto Kuwa Fursa

Usiyaone matatizo katika jamii kama kikwazo kikubwa katika maisha yako. Ni kweli matatizo sio jambo zuri hata kidogo, lakini yanapotokea matatizo au changamoto, usikae kuyashangaa tu. Fikiria ni kwa kiasi gani unaweza kusaidia katika matatizo hayo. Kumbuka unaposaidia watu unaongeza mtandao wa watu unaofahamiana nao na unaokubalika kwao.

Lakini pia, unapoona changamoto katika jamii, fikiria jinsi gani zinaweza kuwa fursa nzuri kwako. Wakati eneo unaloishi linakumbwa na tatizo la maji kwa mfano, fikiria unaweza vipi kuigeuza hiyo kuwa fursa kwako? Kumbuka mahitaji ya jamii ni fursa kubwa kwako.

  1. Tunza Kumbukumbu

Hili watu wengi huwa wanalisahau sana hasa sisi waafrika hususan vijana wengi wa Tanzania. Jiulize wangapi wana ‘Diary’. Swali hilo likihamia kwako pia utabaini kitu. Kama unayo Diary, jiulize unatunza kumbukumbu ya yale mambo unayofikiria kama ‘ideas’ au mambo unayoyafanya?

Je, unatunza kumbukumbu ya mikutano unayofanya na watu mbalimbali kwenye mambo ya msingi? Kumbuka hakuna maendeleo bila kumbukumbu. Kumbukumbu hizo zitakusaidia kuziendeleza kwa kuziboresha ili ziwe kitu kikubwa baadaye. Akili ya binadamu huwa na tabia ya kusahau, hata kama utakuwa unakumbuka, huwezi kukumbuka kile kilichotokea kwa asilimia 100. Hivyo, pale unapotaka kuendeleza wazo lako unapaswa kuwa na kumbumbu muhimu. Kwa wafanyabiashara kumbukeni kuwa ‘mali bila daftari huisha bila habari’.

Cha mwisho na muhimu sana, ni lazima uweke kumbukumbu ya mpango kazi wa siku inahyofuatia ‘To Do List’. Ukiweza kuweka kumbukumbu ya mambo unayotaka kufanya kwa siku inayofuatia utaweza kupanga vizuri ratiba yako na kujipima utekelezaji wake baada ya siku kuisha, huku ukiorodhesha tena mambo ambayo utaanza nayo siku inayofuata.

 

TFF Na Kampeni Za Vyama Vya Siasa
Kompany: Hatuihofii Juventus