Mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, Samuel Sita ameendelea kusisitiza kuwa Edward Lowassa alihusika moja kwa moja na kashfa ya Richmond na kwamba muda wowote serikali inaweza kumfungulia mashtaka mahakamani.

Sitta ameyasema hayo katika kampeni za CCM zinazoendelea mkoani Shinyanga ambapo ameendelea kusisitiza kuwa anahitaji kufanya mdahalo na Lowassa kuhusu Richmond ikiwa ni miaka takribani 8 imepita. Ameeleza kuwa Lowassa aje katika mdahalo huo na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu pamoja na marafiki zake na kwamba yeye atakuwa na Harison Mwakyembe aliyekuwa mwenyekiti kamati maalum ya bunge iliyochunguza sakata hilo.

Sitta ambaye alikuwa spika wa bunge aliyeiteua kamati hiyo ya Mwakyembe, aliwataka wananchi kutomwamini Lowassa akida amejilimbikizia mali miaka miwili tu ya uwaziri mkuu wake. “Kama alikuwa waziri mkuu kwa miaka miwili tu akawa bilionea, akiingia ikulu itakuwaje?” alihoji Samweli Sitta.

Hata hivyo, Edward Lowassa aliwahi kusema kuwa amefunga ukurasa wa kujieleza kuhusu sakata hilo kwa kuwa ameshaeleza mara kadhaa hasa baada ya kujiunga na Chadema, ambapo aliwataka wenye ushahidi wa kashfa hiyo kwenda mahakamani.

“Kama kuna mtu mwenye ushahidi wa Richmond, aende mahakamani, nimechoka kusikia mambo haya,” alisema. “Kama una ushahidi nenda mahakamani, kama hauna keep quiet and shut up!”

Wakati Sitta akiendelea kumundama Lowassa,  mgombea huyo wa urais jana ameendelea na kampeni zake mkoani Iringa huku akiwa akijikita katika kuwaomba kura wananchi wa mkoa huo ambapo aliwataka wananchi hao kutoogopa kufanya mabadiliko. Aliwataka wananchi hao wasiogope kwa kuwa hata Biblia Takatifu imeandika mara nyingi sana neno ‘usiogope’.

Kampeni za uchaguzi mkuu zinaendelea kushika kasi huku vijembe na tuhuma zikitawala wakati mwingine kuliko sera zilizoainishwa kwenye ilani ya vyama hivyo, jambo ambalo limekosolewa na baadhi ya wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa.

Moses Kuihama Chelsea Leo
Dk. Slaa Kupasua Jipu Leo, Kubadilisha Hali Ya Kampeni