Mwanasiasa Mkongwe aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta jana aliweka wazi kuwa amestaafu siasa.

Sitta ambaye hivi karibuni alikatwa mara tatu katika nafasi za siasa kupitia chama chake,  alimwambia mwandishi wa gazeti la Mwananchi kuwa ameamua kustaafu siasa na sasa atajikita katika uandishi wa vitabu na kutoa ushauri.

“Mambo ya kisiasa kwa sasa basi, “alisema Sitta. “Nipo tu nyumbani nimepumzika. Naridhika na niliyoyafanya kwa Taifa. Wale wanaotaka kupata ushauri wakinifuata nitawasikiliza,” aliongeza.

Sitta alisema kuwa vitabu atakavyokuwa anaandika vitakuwa vimebeba mtazamo wake kwa jinsi anavyoyaona mambo ya nchi.

Sitta alikatwa na chama chake katika mbio za kuwania kugombea urais, lakini pia aliporusha kete yake kutaka kuwania uspika wa Bunge kwa tiketi ya Chama chake alikatwa katika hatua za awali licha ya kubainisha kuwa yeye ndiye aliyekuwa na sifa zaidi ya wenzake. Sitta alitahadharisha kuwa endapo utaratibu utakiukwa katika mchakato wa kumpata Spika angeenda Mahakamani lakini bado hakuwa miongoni mwa watatu walioenda katika hatua ya kupigiwa kura.

Jina la Samwel Sitta pia limekosekana kati ya mawaziri wa serikali ya awamu ya Tano wenye sifa za ‘Hapa Kazi Tu’. Huenda ni kutokana na udogo wa baraza lenyewe au nia yake ya kutaka kustaafu siasa.

Uamuzi wa Sitta kustaafu siasa unafanana na ule wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, mwanasiasa machachari Dk. Wilbroad Slaa.

Dk. Slaa alitangaza kustaafu siasa kutokana na kutoridhishwa na utaratibu uliotumiwa na chama chake kumpokea Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea urais.

Ni kama vile Sitta amezifuata nyayo za Dk Slaa ambapo wanasiasa hao wawili wameweka rekodi mwaka huu kwa kutangaza kustaafu siasa licha ya kuwa na ushawishi mkubwa kwa umma.

 

Pius Msekwa adaiwa kudanganya Kuhusu Stori yake na Mwalimu Nyerere
Somalia Yafuta Sherehe za Krismas