Saa chache baada ya tasnia ya habari nchini kupata pigo lingine kubwa kwa kuondokewa na mtangazaji gwiji na maarufu, Ephraim Kibonde wa Clouds FM, meneja wa ubunifu wa kituo hicho cha redio, Siza ameeleza kilichotokea awali.

Siza amesema kuwa Kibonde alianza kujisikia vibaya muda mfupi baada ya kumaliza kutangaza wakati wa kuaga na kumzika Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, Bukoba mkoani Kagera.

Amesema kuwa hali ya Kibonde ilibadilika, akapelekwa ndani ya nyumba ya familia ya Ruge na kupatiwa huduma ya kwanza na wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu, ikiwa ni pamoja na kumlegeza mkanda na kumvua viatu.

Kwa mujibu wa Siza, walimpeleka hospitalini mjini hapo lakini baadaye madaktari wa hospitali hiyo kwa kushirikiana na Dkt. Issack Maro ambaye pia hutangaza Clouds FM walishauriana na kukubaliana kuwa apelekwe jijini Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Baada ya majadiliano tulimuuliza Kibonde kama anaweza kusafiri hadi jijini Mwanza kwa kuwa ndege yetu ilikuwa inaondoka asubuhi, alisema anaweza, tukakubaliana na kumpeleka uwanja wa ndege kwa safari,” Siza ameiambia Mwananchi.

“Baada ya kufika [Mwanza] tulimuacha Kibonde na Dkt. Issack na daktari mwingine ambaye ni rafiki yake sisi tukaendelea na safari yetu kuelekea Dar es Salaam, hadi asubuhi tunapata taarifa amefariki. Hivyo ndivyo ilivyokuwa,” amesema.

Kibonde alikuwa mtangazaji nguli kupitia kipindi cha Jahazi, lakini pia ndiye muasisi wa kipindi cha Sports Extra na mmoja kati ya watu waliobadili hali ya utangazaji wa vipindi va michezo kutoka ‘kutangaza kwa kasi kubwa’ hadi kutangaza kawaida.

Hakika hili ni pigo lingine kubwa kwa tasnia ya habari nchini, Mungu ametoa na Mungu ametwaa, jina lake lihimidiwe.

Kusaga amlilia Kibonde, atangaza ratiba ya msiba
Rais Kagame kufanya ziara nchini

Comments

comments