Uanzishwaji wa vyama vya Umwagiliaji kwa ajili ya usimamizi wa skimu za umwagiliaji ni suluhisho la utunzaji wa skimu hizo itakayosaidia Tanzania kuwa ya viwanda kupitia kilimo cha umwagiliaji.

Hayo yamesemwa mjini Bariadi katika Viwanja vya Nanenane vya Nyakabindi na Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Zukheri Huddi, alipokuwa akizungumza na wakulima na waandishi wa habari waliotembelea banda la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Amesema kuwa Sheria ya Umwagiliaji namba 5 ya mwaka 2013 na kanuni zake za mwaka 2015 inahamasisha skimu za umwagiliaji kusimamiwa na kuendelezwa na vyama vya umwagiliaji ili ziweze kuwa na ufanisi.

Aidha, amesema kuwa ili kilimo cha umwagiliaji kiwe endelevu na chenye tija kuweza kufikia Tanzania ya Viwanda na Biashara, wakulima wote nchini wanaomiliki mashamba katika skimu za umwagiliaji wanatakiwa kujiunga katika vyama vya umwagiliaji.

“Kuanzia tarehe ya kuanzishwa kwa chama cha umwagiliaji, katika skimu husika chama hicho kinatakiwa kusajiliwa chini ya sheria na kanuni za umwagiliaji na wakulima wote watatakiwa kuwa wanachama wa chama cha umwagiiaji na watalazimika kutekeleza masharti ya chama hicho,” amesema Huddi

Hata hivyo, ameongeza kuwa chini ya Sheria ya Umwagiliaji na kanuni zake, imeweka bayana kwamba, chama, taasisi au chombo chochote kinachojishughulisha na shughuli za umwagiliaji kitatakiwa kutuma maombi yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, kwa kujaza fomu ya maombi ya ukubalifu kisha kitapatiwa cheti cha kukubaliwa.

 

Umoja wa Mataifa wainyoshea kidole Korea Kaskazini
NEC yatangaza tarehe ya uchaguzi majimbo ya Ukonga, Korogwe na Monduli