Meneja wa wagonga nyundo wa jijini London (West Ham Utd) Slaven Bilic anaamini matokeo mabaya yanayokiandama kikosi chake katika kipindi hiki cha mwanzoni mwa msimu, ni changamoto za muda mfupi.

Bilic ambaye msimu uliopita alionyesha makali akiwa na wagonga nyundo hao, ameyasema maneno hayo ya kujifariji baada ya kupokea kisago cha mabao matatu kwa sifuri kutoka kwa Southampton katika mchezo wa jana wa ligi kuu ya Uingereza.

Bilic alitumia neno la changamoto za muda, kuwaambia wachezaji wake dakika chache baada ya kukutana katika chumba cha kubadilishia, mara tu, kipyenga cha mwisho kilipopulizwa.

Aliwaambia wanapaswa kushikama na kuamini hakuna njia ya mkato kwa sasa, zaidi ya kuamini wanachokifanya ni kwa ajili ya klabu lakini bahati ya ushindi imekua ikiangukia kwa wapinzani wao.

Mbali na kuwaeleza wachezaji maneno hayo, Bilic aliirudia kauli hiyo ya kujifariji wakati alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Sky Sports dakika chache kabla ya kuondoka Olympic Stadium.

Bilic alisema: “Sisi sio wa kwanza na wala si wa mwisho kukutana na hali kama hii, naamini kila mchezaji wangu anafahamu kinachotusibu kwa sasa, lakini ninatarajia matokeo mazuri siku za karibuni.

“Nimewaambia wachezaji wangu ukweli wa mambo, kuhusu bahati mbaya inayotukuta kwa sasa, lakini hilo kwetu tunalichukua kama changamoto ya kujipanga vilivyo kabla ya kuendelea na mikakati ya kusaka point zitakazoturejesha katika ubora wetu.” Aliongeza Bilic.

Mpaka sasa West Ham Utd imepata ushindi mara moja miongoni mwa michezo sita waliyocheza huku wakipoteza mara tano.

Kevin de Bruyne Aiweka Majaribuni Man City
Angelina Jolie amtoa chozi Brad Pitt, ampa adhabu nyingine nzito baada ya kumtosa