Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalla Ulega amesema Serikali inafanya jitihada ili mwalo wa
wavuvi wa samaki wa Kirando uliopo Wilaya ya Nkasi uweze kufikia hadhi ya kuwa soko la kisasa
la samaki na mazao ya uvuvi.

Ulega ameyasema hayo hii leo Jumatatu Mei 23, 2022 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali
la mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Khenani ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa
kujenga Soko la kisasa la mazao yatokanayo na uvuvi Wilayani Nkasi.

Amesema mpango wa Serikali ni kujenga na kuboresha miundombinu ya uvuvi ikiwemo mialo na
masoko katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo upande wa mwambao wa Ziwa Tanganyika
unaojumuisha Wilaya ya Nkasi.

“Shughuli za uvuvi zinafanyika katika mialo ipatayo 239 na Serikali imeboresha mialo minne ya
Kibirizi Manispaa ya Kigoma ujiji, Ikola Tanganyika, Muyobozi Uvinza na Wilaya ya Kirando
Nkasi,” amefafanua Waziri Ulega.

Aidha Waziri huyo amesema Serikali imejenga na kuboresha masoko mawili ya samaki ya Kibirizi
Mkoani Kigoma na Kasanga ambalo lipo katika wilaya ya Sumbawanga na kudai kuwa suala la
ulinzi wa maeneo ya mazao ya samaki ni jukumu la kila mmoja.

“Ulinzi wa mazalia ya samaki na ulinzi wa maeneo ya mazao ya samaki ni jukumu la kila mtu na
katika hili hatutamfumbia macho mtu yeyote atakayebainika kuhusika kuharibu maeneo ya
mazalia,” amesisitiza Naibu Waziri.

Jay-Z ashutumiwa kutega mtego wa risasi kwa Megan Thee
Rais awataka raia kupambana na hali zao