Meneja wa muda wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid, Santiago Hernán Solari Poggio, amesema hawazii nafasi ya kupandishwa chezo na kuwa meneja wa kudumu, zaidi ya kufikiria namna ya kuisaidia klabu hiyo.

Solari alizungumza jambo hilo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari mara baada ya mtanange wa jana usiku, ambao ulishuhudia kikosi chake kikiibuka na ushindi wa mabao manne kwa mawili dhidi ya Celta Vigo.

Kiungo huyo wa zamani wa The Meringues, alisema itakua ni upuuzi na ujinga kuanza kufikia kazi ya moja kwa moja katika kipindi hiki, ambacho amekabidhiwa jukumu la kuivusha Real Madrid iliyokua ikipita kwenye wakati mgumu.

“Sina nafasi ya kuanza kufikiria ajira ya kudumu, nipo hapa kwa ajili ya kuisaidia Real Madrid ili ifanikishe mpango wa muda mfupi, suala la nani atakaetangazwa kuwa meneja wa kudumu lipo juu ya uwezo wangu.”

“Nilipewa nafasi hii kwa kuaminiwa sana na uongozi, ninapaswa kuiheshimu na kuitumikia kama nilivyoagizwa, atakapo tangazwa mtu mwingine nitaheshimu, ima iwe mimi itakua sawa, na kama sio mimi itakua sawa pia.”

“Jukumu langu kwa sasa ni kuhakikisha tunaendelea kupata matokeo mazuri, na kwa hilo ninaendelea kuwashukuru wachezaji ambao kila siku tangu nilipochukua nafasi hii wamekua wakifuata maelekezo yangu na kuyafanyia kazi katika dakika 90.” Alisema Solari aliyeitumikia Real Madrid kuanzia mwaka 2000–2005.

Oktoba 30 Solari alitangazwa kuwa meneja wa muda baada ya kutimuliwa kwa Julen Lopetegui, na mpaka sasa ameshakiongoza kikosi cha Real Madrid katika michezo minne na kushinda yote.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 13, 2018
Ja Rule ajibu jaribio la 50 Cent kununua haki ya nyimbo zake

Comments

comments