Kocha wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amemvika koti lenye nyota ya ushujaa mlinda mlango David de Gea akidai kuwa anaweza kuwa golikipa bora zaidi kuwahi kuichezea klabu hiyo.

De Gea aliteka usikivu wa Solskjaer baada ya kufanikiwa kuzuia mipira takribani 11 akiisaidia Man United kuondoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Tottenham katika uwanja wa Wembley, jana.

Kocha huyo ambaye enzi zake alipoichezea Man United alifanikiwa kucheza na walinda mlango mahili Edwin van der Sar na Peter Schmeichel, amesema kuwa anaamini De Gea anaweza kuwa mshindani wao mkuu.

“Tumekuwa na walinda mlango bora hapa kwenye Klabu yetu na nafikiri De Gea anaweza kuwa mshindani mkuu wa Edwin van der Sar na Peter Schmeichel, kushika nafasi ya kwanza katika historia,” alisema Solskjaer.

Kiwango cha kuzuia magoli wakati wa mechi kati ya timu hiyo na Tottenham kilikuwa cha juu zaidi katika michezo ya Ligi Kuu akiisaidia klabu hiyo kushinda michezo sita mfululizo ikiwa chini ya Solskjaer.

Mbali na sifa alizomwagiwa na kocha huyo, Peter Schmeichel pia alimvulia kofia De Gea akidai kuwa ulinzi wake wa mlango ni sawa na ukuta.

Mlinda mlango huyo wa Timu ya Taifa ya Uhispania mwenye umri wa miaka 28, alijiunga na United akitokea Atletico Madrid mwaka 2011.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 15, 2019
Kamanda wa Polisi afunguka askari watatu kumpa kibano dereva

Comments

comments