Mshambulaiji wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Son Heung-min huenda akakosa michezo ya awali ya msimu mpya wa ligi kuu ya soka nchini England, kufuatia kujumuishwa kwenye kikosi cha Korea Kusini kitakachoshiriki michezo ya bara la Asia (Asian Games), itakayounguruma Indonesia.

Son amejumuishwa kwenye kikosi cha timu yake ya taifa na kuwa miongoni mwa wachezaji watatu waliovuka umri wa miaka 23 wanaohitajika kikanuni kwenye michuano hiyo, ambayo imepangwa kuanza Agosti 14 na kumalizika Septemba Mosi.

Kikosi cha Tottenham kitaanza kampeni ya kusaka ubingwa wa England msimu wa 2018/19 kwa kucheza dhidi ya Newcastle Utd Agosti 11, kabla ya kupapatuana na Fulham, Manchester United na Watford.

Michezo hiyo itachezwa wakati Son akiwa katika majukumu ya kulitumikia taifa lake kwenye michuano ya michezo ya bara la Asia (Asian Games).

Hata hivyo, michezo wa bara la Asia haipo kwenye kalenda ya shirikisho la soka duniani FIFA, hivyo uongozi wa klabu ya Tottenham utakua na jukumu la kuchagua kumruhusu ama kupinga maamuzi ya shirikisho la soka Korea Kusini, kutumika kwa mchezaji huyo.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Korea kusini chini ya umri wa miaka 23 Kim Hak-bom aliwaambai waandishi wa habari wakati akitangaza kikosi cha wachezaji 20 kuwa, watazishukuru klabu zote zitakazokubali kuwaachia wachezaji aliowaita, ili wacheze kwenye michuano ya Asian Games.

Kwa mantiki hiyo imedhihirika shirikisho la soka Korea Kusini halijafikia makubaliano yoyote na uongozi wa Tottenham Hotspurs kuhusu kuitwa kwa mshambuliaji huyo, na katika kipindi hiki kilichosalia kabla ya kuanza kwa michuano hiyo uongozi utalazimika kutuma maombi ya kutumika kwa Son.

Son alikua sehemu ya kikosi kilichoshiriki fainali za kombe la dunia nchini Urusi, na alifunga mabao mawili.

Marekani yamnyima VISA Alexis Sánchez
Nape ajilipua tena, ‘nyekundu iwe nyekundu’

Comments

comments