Mshambuliaji kutoka Burkina Faso Yacouba Songne huenda akaukosa mchezo wa fainali wa Kombe la Mapinduzi 2021 dhidi ya Simba SC utakachezwa leo usiku Uwanja wa Amaan mjini Unguja visiwani Zanzibar.

Kocha mkuu wa Young Africans Cedric Kaze, amesema mustakabali wa mshambuliaji huyo kucheza mchezo dhidi ya Simba SC utatolewa na madaktari ambao wanatarajiwa kuwasilisha ripoti mchana huu.

Hata hivyo kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema wachezaji wake wote wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo, ambao utanza mishale ya saa mbili na robo usiku.

“Kuhusu wachezaji wangu wote waliopo wapo vizuri na wanaendelea salama, ila ninadhani kwamba mchezaji wetu Yacouba nitasubiri ripoti ya madakatari kwa kuwa alipata majeraha kwenye mchezo wetu uliopita.”

“Ninaamini kwamba tutakuwa na dakika 90 nzuri hivyo mashabiki wasiwe na mashaka sisi tupo vizuri na mwisho matokeo yatapatikana.” Amesema Kaze

Songne aliumia kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali ya kwanza dhidi ya Azam FC wakati Young Africans ikishinda kwa mikwaju ya penati tano kwa nne, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao moja kwa moja ndani ya dakika 90.

Kocha Ibenge aitamani Simba SC, lakini.....
Vikao vya kamati za bunge kuanza January 18