Baada ya kutoa ruhusa ya kuvunjwa kwa mkataba kati yao na meneja kutoka nchini Uholanzi Ronald Koeman ambaye yu njiani kujiunga na klabu ya Everton, uongozi wa Southampton umeanza mikakati ya kumshawishi aliyekua mkuu wa benchi la ufundi la Ajax Amsterdam, Frank De Boer.

Taarifa zilizochapishwa katika gazeti la Daily Mail la nchini England, zimeeleza kwamba, The Saint wametoa nafasi kwa meneja huyo wa kidachi kwa kumtangazia mkataba wa miaka mitatu.

Uongozi wa wa Southamton unaamini De Boer, atakua mtu sahihi wa kuchukua mikoba ya Koeman ambaye alionyesha kukimudu kikosi cha klabu hiyo kwa kufanya vyema na kutoa upinzani wa kweli dhidi ya klabu nyingine za ligi kuu ya soka nchini England.

Hata hivyo mpaka sasa De Boer, bado hajatoa jibu kama amekubaliana na ofa ya mkataba wa miaka mitatu aliyopewa ama la, hivyo uongozi wa The Saint unasubiri jibu kutoka kwake.

Wakati mchakato huo ukiendelea, huenda Southamton wakapata changamoto ya kufanikisha zoezi hilo, kufuatia De Boer kuwa sehemu ya mikakati ya kuwaniwa na klabu ya SS Lazio inayoshiriki ligi ya nchini Italia (Sirie A).

SS Lazio wameanza mchakato wa kumsaka meneja wa kikosi cha kwanza, baada ya kumtimua Stefano Pioli mwezi Aprili mwaka huu na nafasi yake ilichukuliwa na Simone Inzaghi ambaye alipewa jukumu la kuliongoza benchi la ufundi hadi mwishoni mwa msimu wa 2015-16.

Liverpool, West Ham United Zamuwania Thomas Vermaelen
Polisi yamng’ang’ania Mbowe Shinyanga