Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemtaka aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu kuwa na shukurani na kwamba asiusingizie uongozi wa bunge hilo.

Akijibu tuhuma zilizoelekezwa kwa Bunge na mwanasiasa huyo ambaye hivi sasa yuko nchini Ubelgiji, Spika Ndugai alisema kuwa madai yake kuwa hajalipwa posho na mishahara ni ya uongo na anachotaka ni kuzungumziwa na kila mtu.

Akipitia nyaraka kadhaa, Spika Ndugai alisimama ndani ya Bunge jijini Dodoma na kueleza kuwa Lissu amelipwa posho zaidi ya Sh. 300 Milioni, na Mishahara zaidi ya Sh. 200 Milioni lakini akamtaka kukumbuka kuwa anadaiwa zaidi ya Sh. 70 Milioni alizokopa kupitia Bunge hilo.

“Kwa ujumla katika kipindi chote alichokuwa hapa amelipwa zaidi ya Shilingi milioni mia tano… na zaidi, sitaki kutaja ‘figure’, lakini akitaka twende nitazidi kufunguka zaidi,” alisema Spika Ndugai.

“Pia akumbuke kuna mikopo aliyochukua maeneo mbalimbali alipokuwa hapa… ila huko aliko Ubelgiji nataka nimkumbushe kuwa kuna pesa anadaiwa hapa zaidi ya Shilingi milioni 70 alizokopa kwenye mikopo mbalimbali kupitia Bunge. Kwahiyo, anapomtuhumu Ndugai akumbuke kuwa aliko awe anarudisha hela huku,” aliongeza.

Wiki iliyopita, Spika Ndugai alizuia hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kusomwa bungeni baada ya kuwa na tuhuma nyingi alizosema hazikuwa za kweli dhidi ya uongozi wa bunge, mojawapo ikiwa inahusu malipo ya Lissu.

 

Corona Tanzania: Idadi ya waliopona yaongezeka
Nyaraka za FBI zaikaanga FIFA

Comments

comments