Katika hali ya mshangao mashabiki wa soka waliofika uwanja wa Amaan jana jioni kwa ajili ya kuangalia mazoezi ya klabu ya SC Villa Jogoo kutoka nchini Uganda wamejikuta wakiangalia milingoti ya bendera pekee kiwanjani hapo baada ya klabu hiyo kutoonekana.

SC Villa ambayo leo saa kumi alasiri inashuka kiwanjani hapo kuwavaa maafande wa JKU walitarajiwa kufanya mazoezi muda huo lakini wameamua kuutoroka uwanja.

Taarifa za ndani ambazo mtandao huu imezipata ni kuwa Villa walishindwa kufanya mazoezi hayo kutokana na kuchelewa kuingia hapa Zanzibar wakitokea jijini Dar es salam ambapo tokea juzi jioni waliwasili wakitokea nchini kwao Uganda kwa njia ya bara bara.

Hata hivyo tokea kikosi cha klabu hiyo kinaondoka nchini kwao Uganda kulikua na taarifa za utatanishi juu ya kuwasili hapa Zanzibar.

Taarifa za awali ambazo zilikuja kwa njia ya mtandao kupitia Email ya ZFA ni kuwa klabu hiyo ilitakiwa kuwasili juzi majira ya saa tatu na robo asubuhi kwa njia ya anga kupiti Kenya Airways lakini haikuwa hivyo.

Taarifa za mwisho zilionyesha kuwa majogoo hao wa Uganda waliondoka Dar es salam kwa boti ya saa kumi na kuwasili Zanzibar majira ya saa kumi na mbili za jioni ambapo kwa sasa tayari wapo visiwani humo.

Kuchelewa huku kwa Villa ndiyo sababu iliyopelekea kutofanya mazoezi kiwanjani hapo jambo ambalo limewafanya mashabiki kuona kwamba labda timu hiyo haina wasi wasi wowote juu ya mchezo huo wa marejeano ambao unachezwa hii leo.

SC Villa ilishinda mabao 4-0 kwenye mchezo wa awali wiki moja iliyopita nchini Uganda na inahitaji ushindi ama sare ya aina yoyote ili isonge mbele kwenye mashindano hayo ya kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kwa upande wao JKU wanahitaji ushindi wa bao 5-0 kuweza kusonga mbele vinginevyo itaungana na wawakilishi wenzao wa Zanzibar klabu ya Mafunzo kuaga mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho hilo kwa mwaka huu wa 2016.

UVCCM Wamkataa Balozi Mwapachu, wadai ana dhambi ya usaliti
Mshauri mkuu wa Maalim Seif anasa mikononi mwa polisi