Uongozi wa FC Barcelona unatafuta njia mbadala za kumuuza kiungo mshambuliaji kutoka Brazil Philippe Coutinho, ambaye msimu uliopita aliwatumikia mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich.

FC Barcelona wanasaka suluhisho la mchezaji huyo, kufuatia mpango wa kuendelea kusalia jumla Allianze Arena kukwama, kufuatia viongozi wa FC Bayern Munich kuweka ngumu kumsajili moja kwa moja.

Klabu kadhaa za barani Ulaya hususan England zimeonyesha kuwa tayari kumsajili moja kwa moja kiungo huyo, ambaye aliwahi kuitumikia Liverpool kabla ya kutimkia Camp Nou.

Klabu za England zinazotajwa kuwa kwenye mchakato wa kuiwania saini ya Coutinho ni Chelsea, Man United, Totenham na Arsenal.

Taarifa zilizopo kwa sasa ni kwamba Arsenal na Totenham ndio klabu zenye uchu mkubwa wa kuwania saini ya Coutinho, ambaye pia anaona nafasi ya kurudi tena kwenye Ligi Kuu Uingereza, ni fursa ya kipee kwake.

Inasemekana Arsenal wamejipanga kumtoa kiungo wao Matteo Guendouzi na kiasi cha fedha takribani pauni milioni 9 ili kumsajili Coutinho.Ofa hii inaonekana itasaidia pande zote mbili – Arsenal na Barcelona ambao wachezaji hawa wanaonekana kutokuwa kwenye mipango ya muda mrefu ya vikosi hivi.

Uongozi wa Arsenal unasubiri kuiona hatma ya Arsenal katika fainali ya Kombe la FA watapokutana na Chelsea. Endapo Arsenal watafanikiwa kunyanyua kombe hilo, watakuwa katika nafasi nzuri kiuchumi na hivyo bajeti ya usajili itaongezeka kwa kiasi fulani.

Arteta bado anakuwa mwenye mashaka katika hili kwani Juventus nao wanaonekana kuitafuta saini ya Guendouzi. Japokuwa, Arsenal mpango wao wa kubadilishana wachezaji bado upo palepale.Kwao (Arsenal) hii ndio njia pekee ya kuendana na madhara ya kiuchumi yaliyosababishwa na Mlipuko wa Virusi vya Corona duniani.

Arteta anamtizama Coutinho kama mchezaji mwenye faida zaidi kulingana na mfumo wake wa kiuchezaji. Anamtizama Coutinho kama mrithi wa Pierre-Emerick Aubameyang endapo mshambuliaji huyo ataamua kuondoka Emirates.

Pia, hali ya sintofahamu kuhusu hatma ya usajili wa Dani Ceballos anayechezea Arsenal kwa mkopo akitokea Real Madrid, inamuongezea mashaka Arteta katika nafasi hiyo. Endapo Ceballos ataamua kuondoka, Arteta atakosa mtu wa kuziba pengo hilo na hivyo Coutinho kuwa usajili wenye faida zaidi kwa Arsenal.

Arsenal watakuwa uwanjani leo kukipiga dhidi ya Chelsea katika fainali ya Kombe la FA. Ushindi kwa Arsenal ni faida kiuchumi, lakini pia itawapa tiketi ya moja kwa moja kushiriki michuano ya Europa msimu ujao.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 2, 2020
Tuchel afunga ukarasa wa Ufaransa kwa furaha