Mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Togo, Emmanuel Adebayor, yupo kwenye wakati mgumu wa kutocheza michezo ya ligi ya nchini England, baada ya uchaguzi uliofanywa na kituo cha televisheni cha Sky Sports kubaini jina lake halijaorodheshwa kwenye kikosi cha wachezaji 25 cha klabu ya Tottenham Hotspurs kitakachoendelea kusaka ubingwa msimu wa 2015-16.

Spurs wanadaiwa kuliondoa jina la mshambuliaji huyo kwenye kikosi chao ambacho kitapambana kwenye michuano ya ligi ya nchini England msimu huu, kutokana na kuamini huenda angefanikisha harakati zake wa kujiunga na klabu ya West Ham Utd siku ya mwisho ya kukamilishwa kwa usajili.

West Ham tayari walikua wameshaonyesha nia ya dhati ya kumsajili Edebayor lakini walishindwa kufanikisha azma hiyo kutokana na hitaji la mshambuliji huyo la kutaka kulipwa mshahara wa paund laki moja (100,000) kwa juma.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31, hajazungumza lolote juu ya jambo hilo lililofanyiwa uchunguzi, na badala yake ameendelea kukaa kimya na kusubiri lolote litakaloamuriwa dhidi yake.

Kufuatia uchunguzi huo kubaini hivyo, kuna wasi wasi mkubwa kwa Adebayor kukaa jukwani na kuwashuhudia wenzake kwa msimu mzima huku akisubiri nusra ya kusajiliwa hata kwa mkopo, kitakapofika kipindi cha dirisha dogo la usajili mwezi januari mwaka 2016.

Mshambuliaji mzawa Harry Kane, ambaye bado hajafunga bao lolote tangu msimu wa ligi nchini England ulipoanza mwezi uliopita, ameonekana kuwa kikwazo kwa washambuliaji wengine kuendelea kuwepo White Hart Lane kwa kuaminiwa anatosha kuongoza mashambulizi.

Roberto Soldado tayari ameshauzwa kwenye klabu ya Villarreal ya nchini kwao Hispania baada ya meneja wa Spurs Mauricio Pochettino, kusisitiza mshambuliaji huyo alikua hatoshi kutimiza mipango yake.

Samatta: Taifa Stars Bado Ina Tiketi Ya 2017
Van Gaal Akubali Yaishe, Amjumuisha Valdes Kikosini