Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limebuni mkaa mbadala wa makaa ya mawe ujulikanao kwa jina la Rafiki Briquette unaotarajiwa kuuzwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar.

Mkaa huo umewavutia wananchi wengi waliotembelea banda la STAMICO na washiriki wa semina ya mazingira iliyofanyika wakati wa Tamasha la Nane la Biashara linaloendelea katika viwanja vya Maisara, Zanzibar.

Akiongea na washiriki wa semina hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema STAMICO iliona fursa katika taka ngumu ambazo ni mabaki ya madini ya makaa ya mawe yanayochimbwa katika mgodi wake wa Kiwira na kuamua kuzalisha mkaa wa majumbani ili kuongeza nishati mbadala ya kupikia itakayosaidia kupunguza ukataji wa miti.

“Taka ngumu ni fursa ya kiuchumi, vijana wanatakiwa kutumia ubunifu ili waweze kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kuwa wanapoamua kuwekeza katika taka ngumu itasaidia kutunza mazingira, kwa kuyafanya kuwa safi na rafiki kwa wananchi na wawekezaji”. Alisisitiza Mwasse

Ameongeza licha ya mkaa huo kuwa rafiki kwa mazingira bali umechangia kuongezeka kwa viwanda nchini kufuatia ununuzi wa mitambo ya uzalishaji mkaa huo, kutoa ajira na kuongeza pato la Taifa kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Aidha ameipongeza TANTRADE kwa kuendelea kuboresha maonesho haya kwa kuandaa mafunzo na majadiliano mbalimbali yanayowakutanisha washiriki na wadau mbalimbali zikilenga kuleta uchumi jumuishi na endelevu wenye ubunifu kwa maslahi ya Taifa.

Awali Dkt. Mwasse alishiriki katika sherehe za maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uwanja wa Amani na baadaye kushiriki katika semina iliyoandaliwa na TANTRADE na kutumia fursa hiyo kuwapongeza Wanzanzibar kwa kuendelea kuwa na moyo wa uzalendo katika kuyaenzi Mapindunzi Matukufu hususani siku ya Maadhimisho ya sherehe hizo za miaka 58 ya Mapinduzi ambazo zilifana sana.

Kwa upande wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE), Mkurugenzi Mkuu Latifa khamis amesema katika kutekeleza majukumu yake, Tantrade imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mazingira yanalindwa na kutunzwa.

Zaka: Kigonya alistahili kadi nyekundu
Nandy aukana ujauzito