Wanachama wa klabu ya Stand United ya mjini Shinyanga wanatarajia kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchaguza viongozi, katika mkutano mkuu wa uchaguzi uliopangwa kufanyika Juni 26, baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) pamoja na mdhamini wa klabu hiyo Kampuni ya Madini nchini Acacia kutoa masharti yao.

Juni 7, TFF na Acacia waliuandikia barua uongozi wa klabu hiyo kuwataka kufanya uchaguzi huo ili kuwapata viongozi halali watakaosimamia shughuli zote za klabu ambapo kesho mchakato wa utoaji fomu za kuwania nafasi mbalimbali utaanza ambapo zoezi hilo litafungwa Juni 17.

TFF waliuagiza uongozi wa muda uliopo madarakani kuunda Kamati ya uchaguzi ndani ya siku 10 ambayo tayari imeundwa na kuongozwa na Mwenyekiti wakili Paul Kaunda, Ridia Ilunda ambaye ni Makamu Mwenyekiti na wajumbe watatu, Juma Marwa, Hamis Haji pamoja na Hamis Matuba.

Acacia wao walitoa siku 45 klabu hiyo iwe imefanya uchaguzi vinginevyo watajitoa kudhamini na hivyo watatumia siku 14 kukamilisha zoezi zima la uchaguzi kabla ya siku walizopewa kumalizika.

Katibu Mkuu wa kamati ya muda iliyochaguliwa hivi karibuni, Kennedy Nyangi amesema mpaka sasa Stand United ina jumla ya wanachama 180 ambapo wanachama waanzilishi wapo 31 huku wapya wakiwa 149.

”Leo fomu zinaanza kuchukuliwa ambapo zoezi hili litachukuwa muda mfupi kulingana na ratiba tuliyonayo kubana, tusipofanya uchaguzi mapema wadhamini wanaweza kukimbia maana wameandika barua kabis kutaka uchaguzi ufanyike,” alisema Nyangi na kuongeza

”Barua ya TFF ilitupa siku kumi tuwe tumeunda Kamati ya Uchaguzi na kuanza mchakato mzima wa uchaguzi ikiwemo utoaji wa fomu na siku ya uchaguzi lakini Acacia walitoa siku 45 uchaguzi uwe umefanyika vinginevyo udhamini wao utakuwa umefikia kikomo,” alisema.

Makala: Filamu ya Soka ya Brazil inaumiza macho
Jose Mourinho Apanga Kumuhamishia Marco Verratti Old Trafford