Kocha wa Stand United, Patrick Liewig amewatema rasmi wachezaji watano waliokuwa kikosi cha kwanza huku akiingiza wapya watatu kutoka mchangani.

Liewig amewatema Rajabu Zahiri, Haruna Chanongo, Nassoro Masoud ‘Chollo’, Abuu Ubwa na Salum Kamana ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu huku akimvutia pumzi straika wake Elius Maguli ambaye anataka kukaa naye mezani kwa ajili ya mazungumzo ya mkataba mpya.

Liewig anasubiri Maguli arejee kutoka kwenye majaribio yake ya siku kumi katika timu ya Amazulu ya Afrika Kusini ambako alikwenda juzi Jumatatu, mkataba wa Maguli na Stand unamalizika mwezi Agosti. Hata hivyo kuna uwezekano mkubwa wa Maguli kugoma kuongeza mkataba mpya kwani hana mahusiano mazuri ya kazi na kocha wake huyo.

Wachezaji ambao mikataba yao inamalizika na wapo kwenye mipango ya Mfaransa huyo kuongezwa mikataba mipya ni nahodha Jacob Masawe na Seleman Selembe huku waliowasajili kutoka mchangani kupitia programu yao maalumu kati ya Acacia na Sunderland ni kipa Charles Minza, beki wa kati John Mtabesya na straika Adam Salamba.

Mratibu wa timu hiyo, Mbasha Matutu alisema: “Hao wachezaji wapya wametoka kijiji cha Ilogo kinachozunguka mgodi wa Bulyanhulu, wametokana na mpango maalumu wa wadhamini wetu kwa kushirikiana na Sunderland ambapo lengo ni kukuza vipaji kwa vijana.

“Kuna wachezaji watakaosajiliwa wenye uzoefu, ila hao walioachwa ni kutokana na mikataba yao kumalizika na hakuna uwezekano wa kuwaongeza mikataba mipya kwani kocha hatakuwa na mipango nao hapo baadaye, ila Maguli bado tunamuhitaji, akirejea tutazungumza naye ingawa kukubali au kukataa ni hiari yake mwenyewe,” alisema Mbasha.

Randy Lerner Akubali Kunawa, Aipiga Bei Aston Villa
Jogoo Wa Jiji Akubali Kuchinjwa Mjini Basel, Uswiz

Comments

comments