Kikosi cha Stand Utd  leo kitacheza mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Simba SC kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Stand Utd waliosafiri kutoka mkoani Shinyanga, watacheza mchezo huo baada ya kupumzika mwishoni mwa juma lililopita, na lengo lao kubwa waliloweka bayana ni kuifunga Simba SC, ili kusitisha ndoto zao za kutwaa ubingwa msimu huu.

Afisa habari wa Stand Utd Deo Kaji Makomba ameiambia Dar24 kuwa, kikosi chao kimepata nafasi nzuri ya kujiandaa na mchezo wa leo, na wanaamini hawana cha kupoteza zaidi ya kuwaliza Simba SC kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Makomba amesema wanaiheshimu Simba SC kama timu kongwe, lakini linapokuja suala la kupambana uwanjani wanaiona timu hiyo ni ya kawaida, kutokana na kuwa na sifa sawa na za timu nyingine ambazo wameshacheza nazo katika mshike mshike wa ligi kuu msimu huu.

“Tupo vizuri, tumejiandaa vya kutosha na tuna uhakika mkubwa wa kufanya kweli leo kwenye uwanja wa Taifa, hilo halitojificha cha msingi ninawaomba wadau wa soka kuutazama mchezo huo ili wajihakikishie ni vipi tutakavyo wanyamazisha wanamsimbazi wenye ndoto za ubingwa.”

“Tulipanga kuwafunga katika mchezo wa mkondo wa kwanza kule kwetu Shinyanga, lakini walichomoka kwa bahati ya bao moja walilotufunga kwa penati, ambayo kwa maoni yangu mimi haikuwa sahihi kutokana na mazingira yaliyosababisha mkwaju huo upigwe, lakini naamini leo 40 za Simba zimetimia.” Deo Kaji aliiambia Dar24.

Tayari Stand Utd imeshajiokoa katika janga la kushika daraja baada ya kujikusanyia point 35 ambazo haziwezi kufikiwa na timu zinapigania kubaki ligi kuu kwa msimu ujao.

Mchezo mwingine wa ligi kuu ya soka Tanzania bara unaochezwa hii leo, ni kati ya Azam FC ambao watawakaribisha Toto Africans kutoka Mwanza.

Profesa Jay azungumzia ushauri wa Mwakyembe kuhusu wasanii kuacha kuimba siasa
NI Manchester United Na Ajax Amsterdam Fainali Europa League

Comments

comments