Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kinachojinoa nchini Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya kuikabili Nigeria, kimepoteza mchezo wake wa kirafiki dhidi Libya baada ya kukubali kipigo cha 2-1.

Katika mchezo huo mkali ulifanyika Kartepe, Uturuki, Libya ilikuwa ya kwanza kutikisa nyavu za Stars katika kipindi cha kwanza, bao lililodumu katika kipindi chote cha kwanza.

Nyota ya stars ilianza kung’aa baada ya John Bocco kusawazisha katika dakika ya 58, hali iliyoongeza morali kwa wachezaji wa Stars walioongeza mashambulizi dhidi ya Libya.

Hata hivyo, kosa moja lililofanywa na Nduda liliipa nafasi Libya kucheka na nyavu za Stars kwa mara ya pili na kuififisha nyota ya ushindi ya kikosi hicho kinachonolewa na Charles Mkwasa. Baada ya kupata bao la pili huku ikilionja joto la mashambulizi ya kikosi cha watoto wa Kikwete, Libya iliamua kurudi nyuma na kuweka ukuta mnene uliodumu kwa mafanikio hadi mwisho wa mchezo huo.

Mchezo huo wa kirafiki ulikuwa sehemu ya ratiba ya Stars iliyo chini ya Mkwasa kujipima maendeleo ya maandalizi yake kabla ya kukikwaa kikosi cha Nigeria Septemba 05, mwaka huu katika mchezo wa kuwania kufuza kwa Mataifa ya Afrika mwaka 2017.

Nay Wa Mitego, Roma Mkatoliki Kunogesha Kampeni Za Ukawa Jumamosi
Makundi Ya Ligi Ya Mabingwa Wa Ulaya Yaanikwa