Ujenzi wa stendi mpya ya mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani katika eneo la Mbezi Luis jijini Dar es salaam unaoigharimu Serikali shilingi Bilioni 50.9 umefikia asilimia 57 na umebakiza miezi minne kukabidhiwa.

Ambapo mkandarasi aliyepewa kazi hiyo ya ujenzi wa stendi kutoka Kampuni ya Hainan International ya China ametakiwa kuongeza kasi ili kufikia lengo lililowekwa na serikali.

Stendi hiyo itakakuwa na uwezo wa kuchukua mabasi zaidi ya 700 kwa wakati mmoja, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mabasi 400 ya stendi ya Ubungo.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga alipotembelea stendi hiyo mwishoni mwa wiki, na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo.

Aidha, Ujenzi wa stendi hiyo ya kisasa, unahusisha sehemu za kuegesha mabasi, magari madogo, maduka makubwa, zahanati, kituo cha polisi na huduma nyingine mbalimbali.

Nyamhanga amesema kukamilika kwa stendi hiyo, kutafungua fursa zaidi za usafiri na biashara kati ya Tanzania na nchi zingine za jirani..

Pia amesisitiza matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi huo. Alisema hatarajii kuona ufujaji wowote na kumtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana ambaye ndiye msimamizi mkuu wa ujenzi huo, kuhakikisha fedha zilizotolewa katika ujenzi huo, zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Sipendi kuona kuna matumizi mabaya ya fedha katika ujenzi huu, nasikia kuna makadirio mapya yamefanyika kutokana na ujenzi wa barabara ya Morogoro, kama kuna fedha zitabaki ijulikane, lakini kama kuna fedha itahitajika kuongezwa ijulikane, kikubwa ujenzi huu ukamilike ndani ya wakati bila kuwepo kwa visingizio vyovyote,” alisema Nyamhanga.

TMA yatabiri mvua kubwa kunyesha siku tatu mfululizo
Marekani na Taliban wakamilisha mkataba wa amani