Washika bunduki wa kaskazini mwa jijini London (Arsenal), wametangaza kumsajili beki kutoka nchini Uswiz Stephan Lichtsteiner akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC.

Lichtsteiner amejiunga na Arsenal kama mchezaji huru, huku mkataba wake na klabu ya Juventus FC ukitarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa mwezi huu.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 34, anaaminiwa huenda akaleta changamoto mpya katika kikosi cha Arsenal kwa kutumia uzofu alionao, jambo ambalo mashabiki wa The Gunners wanalisubiri.

Baada ya kukamilisha usajili wake huko kaskazini mwa jijini London Lichtsteiner alisema: “Ninajihisi furaha kuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal!

“Nitashirikiana na wenzangu ili kuleta matokeo chanya kwa msimu ujao, ninaamini hakuna litakaloshindikana, kwa sababu klabu hii ina kiu ya kusaka mataji.”

Lichtsteiner anakua mchezaji wa kwanza kusajiliwa klabuni hapo chini ya utawala wa meneja mpya Unai Emery, na amekabidhiwa jezi namba 12.

Kocha wa Arsenal Emery amesema: “Stephan ataleta mabadiliko kwenye kikosi, kutokana na uzoefu mkubwa alionao, nimemfuatilia kwa muda mrefu, nimebaini ana uwezo mkubwa wa kupambana na kuwahamasisha wachezaji wenzake kuwa kwenye mlolongo wa kutokukata tamaa.”

Lichtsteiner ameondoka Juventus huku akiacha kumbukumbu ya kucheza michezo 250, na kwa upande wa timu yake ya taifa ambayo itashiriki fainali za kombe la dunia 2018, ameshacheza michezo 99.

Ametwaa mataji saba ya ligi ya nchini Italia (Serie A), mataji manne ya kombe la Italia (Coppa Italia) na mataji matatu ya Italia Super Cup, akiwa na klabu ya Juventus, ambayo ilimsajili mwaka 2011 akitokea SS Lazio.

Mamba amuua mchungaji akiwabatiza waumini ziwani
Magazeti ya Tanzania leo Juni 6, 2018