Unaweza kumuita rapa ‘ambukizi wa mtindo wa kuchana’ (Stereo flow) ulioiteka mitaa na kuigwa na wasanii wengi chipukizi mwaka 2011 alipoachia wimbo wake ‘Nitabaki Juu’. Lakini mwishoni mwa mwaka jana mapenzi yalimtoa juu na kumshusha chini alipotulia na kueleza hisia zake hadharani kwa rapa Chemical.

Inawezekana shughuli ya kuchora ‘mistari konde’ ya Stereo ilikuwa sio ngumu sana kama shughuli aliyokutana nayo ya kuchora mistari halisia kumueleza mchora mistari mwenzake, Chemical kile kinachousumbua moyo wake.

Akifunguka kupitia kipindi cha Ladha 3600 cha E-FM kinachoongozwa na Jabir Saleh, Stereo alifunguka kwa moyo uliopondeka akimtumia ujumbe Chemical, ujumbe ambao hata hivyo uliufikia umma moja kwa moja.

“Mimi ni mwanaume lijali kabisa, mwenye sound mind, mwenye haiba yangu, I know what I want… I know what I feel. Inaweza kuonekana kama ni kitu fulani cha ajabu kweli lakini ndivyo ilivyo, kila shetani ana mbuyu wake mazee!” Stereo alieleza katika ujumbe wake huo kwa Chemical ambaye ndiye mbuyu wake sasa.

Akishusha pumzi nzito, Steereo ambaye huenda alipitwa na kauli ya Chemical aliyowahi kueleza hivi karibuni kuwa yeye hajawahi kumjua mume (ni bikira haswaa), alieleza kuwa mapenzi yake kwa rapa huyo hayana masharti na haijalishi alishawahi kuwa na wangapi.

“I don’t care about your past, hata kama ulishawahi kuwa na wanaume 100… lakini naamini kwa kile ninachokihisi sasa hivi,” alifunguka zaidi memba huyo wa zamani wa Lunduno.

Hata hivyo, Stereo anajua kucheza na demokrasia ya mapenzi, ingawa moyo wake una mzigo mkubwa wa hisia nzito za mapenzi kwa Chemical, bado alieleza kama mgombea wa jimbo aliyekomaa kisiasa kuwa atakubaliana na matokeo yoyote.

“Pia, kama ukisema ‘Yes’ ni sawa tu, na ukisema ‘No’ pia ni sawa kwa sababu sio lazima, katika hali ya kawaida ya maisha kila mtu ana vipaumbele vyake na kila mtu ana vitu vyake ambavyo anavipenda kwa mtu mwingine,” alisema.

Ingawa baadhi ya watu walimkosoa Stereo kwenye mitandao ya kijamii kuwa ameshindwa kumfuata rapa huyo hadi ameamua kutumia vyombo vya habari, ujumbe wa Stereo ulimfikia mlengwa kwa ‘surprise’ ya aina yake na kushindwa kueleza majibu.

“Imekuwa surprise sana kwangu, sikutegemea…” alisema Chemical ambaye hata hivyo hakutoa matokeo ya uamuzi wake kwa mgombea binafsi wa jimbo lake la mapenzi, Stereo aka SingaSinga.

Itakuwaje mwaka huu, tusubiri uamuzi wa mmiliki wa jimbo la mapenzi, kwa mgombea wake. Kuna jamaa (sio mhenga) anadai kama mapenzi ni kikohozi basi stereo alikubwa na kubanja, asingeweza kuficha kishindo. Ya Ngoswe tumuachie Ngoswe, utapata majibu hapa hapa Dar24.

TRA yanasa wakwepa kodi jijini Dar es salaam
Picha: Waziri Nchemba akutana na Mama Chid Benz, aeleza alivyoguswa