Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City Raheem Sterling, ametishia kuachana na klabu hiyo endapo hatapewa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha Pep Guardiola.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26, lengo lake ni kutaka kuendelea kuwa mchazaji mwenye kipaji cha hali ya juu, na anaamini hilo haliwezi kufanikiwa kama, atakosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Sterling, ambaye mkataba wake utafikia kikomo mwaka 2023, amesema kwamba alikuwa na ndoto ya kucheza soka nje ya England tangu akiwa mdogo, hivyo kama atashindwa kutimiziwa matakwa yake, atakuwa tayari kuondoka.

‘’Iwapo kungekuwa na fursa kwenda kwingine, ningekuwa tayari kufanya hivyo. Kwa sasa soka ndicho kitu muhimu kwangu. Nimekuwa na malengo ya kucheza ugahibuni ili kupata changamoto mpya,’’ amesema Sterling.

Sterling alianzishwa katika mchezo mmoja ligi kuu ya England, japokuwa alianzishwa kwenye kikosi cha kwanza cha Manchester City katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya PSG, Septemba 28.

Kusajiliwa kwa kiungo Mshambuliaji kutoka England Jack Grealish kutoka Aston Villa kwa dau la Pauni milioni 100 kumeongeza ushindani kwenye nafasi za washambuliaji klabuni hapo, japokuwa kutokuwepo kwa Ferran Torres kwa takriban mwezi mmoja baada ya kupata jeraha la mguu kumepunguza chaguo la Guardiola.

Sterling alijiunga na Manchester City akitokea Liverpool mwaka 2015, na amefanikiwa kushinda mataji matatu ya ligi ya England, Kombe la FA na kushinda Kombe la Ligi (Carabao Cup) mara nne.

Simba yashtukia hujuma Botswana
Kenya: Mume wa mwanariadha aliyeuawa kwa kuchomwa kisu akamatwa