Klabu ya AS Roma ya Italia imethibitisha kumsajili kiungo kutoka Ufaransa Steven NZonzi akitokea Sevilla ya Hispania, kwa ada ya Euro milioni 30.

N’Zonzi mwenye umri wa miaka 29, amejiunga na wababe hao wa mjini Roma, na kusaini mkataba wa miaka minne ambao utamuweka Stadio Olimpico hadi mwaka 2022.

Kiungo huyo anaondoka Hispania baada ya kucheza soka kwa misimu mitatu akiwa na Sevilla, na alikua miongoni mwa wachezaji walioiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Europa League msimu wa 2015-16.

“Nimefurahishwa na hatua ya kujiunga na klabu ya AS Roma, nimeridhishwa na mazingira ya klabu hii, ninaamini yataniwezesha kucheza soka la ushindani na kusaidia malengo yanayokususdiwa kwa msimu ujao,” Alisema Zonzi alipokua akihojiwa kwenye kituo cha televisheni cha Roma TV.

“Niliposikia AS Roma wana mpango wa kunisajili, sikusita kulikubali jambo hilo, nilitambua ninakuja katika mahala ambapo nitakua salama na nitafikia mipango niliojiwekea ya kupambana kikamilifu na kucheza katika kikosi cha kwanza.”

“Sina budi kusema ahsante kwa kila mmoja aliyefanikisha mafanikio yangu katika soka, hususan mkurugenzi Monchi ambaye alinipeleka Sevilla na kunisaidia mambo mengi katika uchezaji wangu. Leo nipo naye tena katika klabu nyingine, hii ni furaha kubwa sana kwangu.

“Malengo makubwa nikiwa hapa ni kutwaa mataji, kucheza kwa kujituma wakati wote kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu, ninaamini yote yanawezekana kutokana na klabu ya AS Roma kuwa na mipango mizuri.”

Nzonzi alijiunga na Sevilla mwaka 2015, baada ya kucheza soka nchini England kwa muda wa miaka sita akiwa na klabu za Blackburn Rovers na Stoke City.

Mwingine upinzani akimbilia CCM
Waziri Kigwangalla afanyiwa upasuaji