Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa michuano waliyoenda kushiriki nchini Zambia, itawasaidia kwa kiasi kikubwa kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC mpaka sasa ikiwa imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi inabanana kileleni na vinara wa ligi hiyo, Yanga wote wakiwa na pointi 39, wakizidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa (Goal Differences), zote zikiwa hazijapoteza mchezo hata mmoja.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz kabla timu hiyo haijaondoka nchini usiku wa kuamkia leo, Hall alisema mbali na kujiandaa na ligi, pia yatawasaidia kuwajenga kabla ya kuvaana na Bidvest Wits ya Afrika Kusini katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwa soka la timu za kusini mwa Afrika linafanana.

“Tunaenda Zambia, hivyo maandalizi yetu ya mzunguko wa pili wa ligi yanatarajia kuwa mazuri kutokana na mechi tatu tunazocheza kule. Mechi tatu za Zambia zinatarajia kuwa ngumu, tutacheza na Zesco United na Zanaco, ambazo zote zinaiwakilisha Zambia kwenye michuano ya Afrika, pia tutacheza na Chicken Inn kutoka Zimbabwe ambao wataiwakilisha nchi hiyo kwenye michuano ya kimataifa (Ligi ya Mabingwa Afrika).

“Hivyo mechi hizo tatu zitakuwa ngumu na itakuwa ni michuano mizuri kwa ajili ya mechi zetu tutakaporejea tutakazocheza dhidi ya Mwadui na Stand United, hivyo tunatakiwa tufanye kazi kwa bidii kwenye hizo mechi,” alisema.

Hall aliongeza kuwa: “Pia itatusaidia kwa kiasi kikubwa kwenye ushiriki wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwa tutacheza na timu kutoka kusini mwa Afrika, ambao mpira wao unafanana, hivyo mechi hizo tatu zitatusaidia kwa kweli.”

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, itaanza kuwania taji la michuano hiyo kesho saa 10.00 jioni kwa saa za hapa kwa kucheza na Mabingwa wa Zambia na wenyeji wao, Zesco United mchezo utakaotanguliwa na ule wa ufunguzi utakaoanza saa 8.00 mchana baina ya Zanaco FC ya huko na mabingwa wa Zimbabwe Chicken Inn.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati watateremka tena dimbani saa 8.00 mchana Jumamosi ijayo kwa kukipiga na mabingwa wa Zimbabwe Chicken Inn, huku ukifuatiwa na ule baina ya wapinzani wa nchini humo Zesco na Zanaco utakaopigwa saa 10.00 jioni.

Azam FC itamalizia mechi yake ya mwisho Februari 3 mwaka huu kwa kukipiga na Zanaco, mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni, utakaotanguliwa na ule baina ya Zesco na Chicken Inn utakaoanza saa 8.00 mchana kabla ya siku inayofuata Februari 4 kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam.

Picha: Mbuzi ajiunga Rasmi na Jeshi la Uingereza na Kupiga gwaride
Man Utd Wakanusha Uvumi Kuhusu Van Gaal