Timu ya taifa ya Uruguay imetupwa nje ya michuano ya Copa America, ikiwa ni baada ya kucheza mechi mbili tu.

Straika wa West Brom Salomon Rondon ndiye aliyeibuka shujaa kwa upande wa Venezuela katika mchezo uliopigwa huko Philadelphia.

Uruguay wamepoteza michezo yote miwili ya kundi C, mchezo uliopita walifungwa na Mexico.

Straika wa Barcelona Luis Suarez alishindwa kucheza katika mchezo wa fungua dimba dhidi ya Mexico kutokana na kusumbuliwa na majeraha aliyopata kwenye fainali ya Copa del Rey mwezi uliopita.

Ilisadikika kwamba, Suarez angekuwepo mchezo wa jana dhidi ya Venezuela hasa pale ambapo walikuwa nyuma kwa goli moja huku wakitaka kusawazisha.

Edinson Cavani alikosa nafasi nyingi za wazi na hata hivyo mpaka sasa hajafunga goli lolote katika michuano hiyo. Amekuwa akishutumiwa kukosa makali yake ya awali kama wakati akikipa kunako klabu ya SS Napoli. Pengine kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara katika klabu yake ya PSG ndiyo sababu kubwa ya straika huyo kukosa umakini golini.

Zikiwa zimesalia dakika 15 tu kabla ya mchezo kumalizika, Luis Suarez alianza kupiga jalamba ili kuingia kuokoa jahazi la Uruguay ambalo lilikuwa likielekea kuzama licha ya kutokuwa fiti kwa asilimia 100.

Lakini baadaye aliambiwa na kocha wake Oscar Tabarez kwamba asingeweza kuingia kwasababu tayari alishaorodheshwa kwenye majina ya wachezaji majeruhi.

Baada ya kocha wake kumwonesha ishara ya kutompa nafasi ya kucheza, Suarez alifanya kituko cha aina yake baada ya kuvua na kutupa kikoi chake na kupiga ngumi katika kuta ya eneo maalum la kukalia benchi la ufundi.

Gozi Hili Kuanza Kupigwa Hii Leo Nchini Ufaransa
Video: Mayweather amsifu Justin Bieber kwa kupigana na Shabiki aliyemzidia