Serikali ya nchi ya Sudan imelishutumu jeshi la Ethiopia kwa kuwanyonga wanajeshi wake saba na raia mmoja aliyechukuliwa kama mfungwa, na kuahidi kulipiza kisasi dhidi ya kitendo hicho.

Kwa mujibu wa Afisa mmoja wa jeshi la Sudan, Ahmed Aidal amesema wanajeshi hao walikamatwa katika eneo la mpakani karibu na mji unaodhaniwa kuwa ni wa Al-Fashagana kuadi hawatatia uoga wa kufanya malipizi ya tukio hilo.

“Katika kitendo ambacho kinakiuka mikataba yote ya vita na sheria za kimataifa, jeshi la Ethiopia liliwanyonga wanajeshi saba wa Sudan na raia mmoja ambao walikuwa mateka wao, hii si sawa na hatutakaa kimya ni lazima kulipiza,” alisema afisa huyo wa jeshi la Sudan.

Mzozo wa mpaka kati ya Sudan na Ethiopia, kuhusu ardhi yenye rutuba katika eneo kubwa la El-Fashaga lililopo jimbo la Gedaref mashariki mwa Sudan, umekuwa kikwazo kikubwa na cha muda mrefu kati ya nchi hizo mbili za Afrika Mashariki.

Migongano baina ya nchi hizo, wakati mwingine hutokea mara kwa mara huku ikiarifiwa kuwa uhasama uliongezeka zaidi mwaka wa 2020 na vita kati ya serikali ya shirikisho ya Ethiopia na mamlaka ya kikanda huko Tigray, ambayo ilisababisha makumi ya maelfu ya Waethiopia kukimbilia Sudan mashariki.

Ingawa wakulima wa Ethiopia wamekuwa wakiishi katika eneo la El-Fashaga kwa miongo kadhaa, lakini inasadikika wanajeshi wa Sudan waliingia tu baada ya mzozo wa Tigray kuzuka huku Ethiopia ikiwa haijajibu kitu kuhusu shutuma hizo.

Mzozo huu wa mpaka, unachochea mvutano kati ya nchi hizo mbili, ambazo licha ya vikao vingi vya mazungumzo hazijawahi kufikia makubaliano juu ya kuainisha mpaka wao na inasemekana Khartoum na Addis Ababa pia zimekuwa katika mzozo kwa zaidi ya miaka 10 kuhusu suala la Bwawa Kuu la Renaissance (GDR) lililojengwa na Ethiopia.

Patrice Lumumba 'kuzikwa' kishujaa DRC
Serikali 'yakunjua makucha' biashara haramu, ujangili