Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao cha dharura kuzungumzia mapigano yanayoendelea  nchini Sudan Kusini.

Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezielezea ghasia hizo zilizoanza tena Sudan kusini, kuwa hazina  sababu na hazikubaliki huku akiwataka viongozi hao kuyaagiza majeshi yao kujiondoa katika mapigano.

Mapigano hayo ni kati ya vikosi vinavyomuunga mkono Rais wa nchi hiyo Salva Kiir na yale yanayoongozwa na Makamu wa Rais Riek Machar.

Mamia ya Watu wameuawa tangu kuanza kwa mapigano hayo wiki iliyopita hadi sasa, katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba.

Viongozi hao wawili hivi karibuni walisaini makubaliano ya amani ya kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka miwili.

Kwa upande wake Mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Sudan kusini Shantal Persaud amesema kambi za pande zote mbili mjini Juba zimeshambuliwa na silaha nzito hali ambayo inatishia mamia ya raia kuwa wakimbizi.

Katibu Mkuu huyo amesema Umoja  wa Mataifa kwa upande wake unasalia na Sudan Kusini na pande zote zinazosaidia nchi hiyo kurejea katika amani na utulivu.

BBC

Nadir Haroub: Iwe Isiwe Medeama Lazima Wakae Taifa
Bajaji, Pikipiki, trekta kuanza kutengenezwa nchini