Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameagiza hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi kuondolewa katika kumbukumbu za Bunge.

Hayo yamejiri leo Bungeni Aprili 18, 2019 ambapo Mbilinyi (Sugu) amegoma kusoma hotuba yake Bungeni kwa madai kuwa zaidi ya 80% ya maneno yameondolewa katika hotuba yake kuhusu bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Sugu amelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson kumtaka asisome baadhi ya maeneo yaliyoko katika hotuba yake. Kwa mujibu kwamba kuna mambo yaliyoondolewa baada ya kuonekana yanakiuka kanuni za kudumu za Bunge.

Kabla ya Sugu kuchukua uamuzi huo, alianza kusoma hotuba kupitia katika kitabu alichokuwa nacho lakini baada ya muda mfupi tangu alipoanza kusoma, Dk Tulia alimtaka asiisome bali asome kupitia kitabu kipya cha hotuba yake ambacho wabunge wote walikuwa wamegawiwa.

Kutokana na maelekezo hayo, Sugu alisema hawezi kufanya hivyo kwani kitabu kipya hakina maoni ya kambi yake na hivyo kulazimika kuondoka mbele ya Bunge na kurudi katika kiti chake.

 

Mamillioni yamiminika dukani kwa Nipsey Hussle
Rais ajiua kukwepa mikono ya polisi