Kiungo kutoka nchini Ghana na klabu ya Pescara ya Italia Sulley Ally Muntari, amesema hatokaa kimya katika suala la ubaguzi wa rangi, ambalo linawakabili wachezaji Kiafrika na wenye asili ya Afrika duniani kote.

Muntari, ambaye alifungiwa mchezo mmoja na shirikisho la soka nchini Italia kufuatia sakata lake la kumtaka mwamuzi asimamishe mchezo ambao uliihusisha klabu yake dhidi ya Cagliari majuma mawili yaliyopita, kufuatia baadhi ya mashabiki wa timu pinzani kuonyesha vitendo vya kumbagua, amesema endapo atakaa kimya kwa kuhofia kuadhibiwa atakua mpuuzi na msaliti kwa waafrika wenzake.

Amesema kwa upande wake, anaamini hali ya kubaguliwa imeshazoeka kwa sababu kila kukicha amekua akikutana nayo huko barani Ulaya, lakini harakati zake za kupingana na ubaguzi anaziendeleza ili kuwaokoa wachezaji wenye umri mdogo ambao wana ndoto za kwenda sehemu za dunia kucheza soka na michezo mingine.

Kuhusu kuunganisha nguvu na wachezaji wengine wanaopinga suala la ubaguzi wa rangi michezoni, Muntari amesema nafasi hiyo ipo, na amewataka wasisite kufanya hivyo kutokana na janga hilo ambalo ameliita “ugonjwa” kuendelea kushamiri katika nchi mbalimbali za barani Ulaya.

Kwa upande mwingine, Muntari amewasihi vijana wa kiafrika na wenye asili na bara la Afrika, kuendelea kuwa na ndoto za kucheza michezo yote kila kona ya dunia, na endapo watakutana na ugonjwa wa ubaguzi, wasisite kuukemea kwa kuwaambia wazi wenye tabia chafu ya kubaguana kwa misingi ya rangi.

Wakati huo huo Sulley Muntari amegomea tuzo ya kupinga ubaguzi wa rangi aliokua ametayarishiwa na kituo cha televisheni cha satirical TV cha Italia.

Muntari alikataa katakata kupokea tuzo hiyo kutoka kwa mtangazaji wa kituo hicho, aliyekua anamsubiri katika eneo la uwanja wa mazoezi wa klabu ya Pescara, ambapo mchezaji huo kutoka Ghana alivyoona kero ya kuombwa kupokea tuzo hiyo inazidi, alivaa Head Phone zake na kuendelea na safari ya kuelekea eneo la uwanja.

Vijana watakiwa kujifunza historia ya nchi na viongozi wao
Gidabudai: Tupo Tayari Kwa Michuano Ya Afrika Mashariki Na Kati