Siku moja baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutangaza nia ya Serikali kumnyang’anya shamba Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, mwanasiasa huyo mkongwe amedai hilo halimtikisi.

Sumaye ambaye tayari ameshakabidhiwa notisi ya siku 90 kutokana na kutoliendeleza, amesema kuwa tayari suala hilo ameshaliwasilisha mahakamani na kwamba mwanasheria wake ndiye anayefahamu tarehe iliyopangiwa kesi hiyo.

“Nilienda mahakamani na ikaamuriwa kusiwe na shughuli yoyote, nasubiri tarehe ya kesi ambayo mwanasheria wangu ndiyo anaijua,” Sumaye anakaririwana MwanahalisiOnline.

Mwanasiasa huyo aliyehamia Chadema miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka jana, amesema kuwa kama CCM wanataka kumdhoofisha kwa kumnyang’anya mashamba ili arejee haitawezekana.

“Kama walidhani kwa kunifanyia hivi nitarudi Chama Cha Mapinduzi (CCM) wasahau, hata kama nilikuwa na nia hiyo sirudi,” amesema Sumaye.

Serikali imetangaza kuanza mchakato wa kumnyang’anya Sumaye shamba lake lililoko Mwabwepande jijini Dar es Salaam kwa madai kuwa ameshindwa kuliendeleza kwa muda mrefu, kinyume na matakwa ya sheria.

Lucas Perez Kuikosa Sunderland
Usingizi wamzidi nguvu Rais Zuma bungeni