Zikiwa zimebaki siku 13 kabla ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ameitumia kashfa ya Richmond iliyopelekea mgombea urais wa Chadema kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu mwaka 2008, kama kete dhidi ya CCM.

Akiongea jana katika mkutano wa kampeni wa mgombea huyo uliofanyika katika jimbo la Tarime Mjini, Sumaye alisema kuwa Lowassa sio mhusika wa Richmond bali wahusika wako CCM.

“Richmond mbona ni ya kwao! Lowassa ametoka walipomwambia. Ili kumuokoa Kikwete na aibu akajitoa kwenye uwaziri mkuu. Lowassa ameondoka bado wakaendelea kulipa Richmond kwa jina la Dowans. Kama ni ya Lowassa kwa nini wanaendelea kuilipa? Wameilipa mpaka juzi.

“Wasimsingizie mtu wa watu kwa sababu ni mtaratibu tu huwa hapendi kujitetea, amenyamaza, kaona Mungu atalipa, Mungu si ndio hii analipa hivi (anaonesha umati uliohudhuria mkutano huo).

Mwaka 2008, Kamati Maalum ya Bunge iliyoundwa chini ya uenyekiti wa Harison Mwakyembe kuchunguza sakata hilo. Kati ya mapendekezo yake, ilimtaka Edward Lowassa aliyekuwa waziri mkuu kujitathmini na kujiwajibisha.

Lowassa aliamua kujiuzulu japo alikanusha tuhuma hizo na kuonesha kusikitishwa na utaratibu uliotumika kutoa pendekezo hilo hasa kwa kuwa kamati hiyo haikumhoji ili kupata utetezi wake dhidi ya tuhuma hizo.

Alisema kuwa anaamini tatizo ni uwaziri mkuu aliokuwa nao hivyo aliamua kujiuzulu.

 

 

Mengi Akanusha Taarifa Zilizosambazwa Kuhusu Yeye Na Lowassa
Mbowe Amfungulia Mlango Dk. Slaa, Atoa Siri Ambayo Hakumwambia Lowassa