Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Sven Vandernbroeck amevishutumu baadhi ya vyombo vya habari kwa kusema vimekua vikiwakosoa wachezaji wake kila kukicha, hasa wanapopata matokeo tofauti.

Sven ametoa shutuma hizo alipozungmza na wadishi wa habari mara baada ya mchezo wa kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Majimaji FC, uliochezwa jana usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amesema mbali na vyombo vya habari, tabia hiyo ipo kwa baadhi ya mashabiki, watu wa ndani na nje ya klabu, jambo ambalo amesema sio la kiungwana.

Amesema kuna haja ya kila mmoja anaejihusisha na tabia hiyo kuiacha, kwa sababu, anafahamu ni vipi wachezjai wake wanavyojitoa kwa 100%, kwa ajili ya klabu ya Simba SC, ambayo msimu huu ina majukumu ya kutetea taji la Ligi Kuu, kutetea ubingwa wa ASFC pamoja na kuwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Amesema badhi ya wachezaji wake wanakosolewa wamekua kwenye wakati mgumu wa kuuguza majeraha, hali inayowapa wakati mgumu wa kuonekana kwenye viwango vyao vya kawaida ama vilivyozoeleka.

“Tangu tukiwa Nigeria, kuna wachezaji walikuwa wagonjwa! Hakukuwa na mchezaji hata mmoja ambaye alikuwa salama katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.”

“Haijalishi wakiwa wagonjwa au wakiwa na afya, wamejitoa kwa kila kitu kupigania klabu pamoja na jezi yake.”

“Sasa naomba VYOMBO VYA HABARI, MASHABIKI, WATU WA NDANI NA NJE YA KLABU kuacha kukosoa kwa sababu hawa vijana wanajitoa kwa kila kitu kwa ajili ya klabu.”

“Badala ya kukosoa wachezaji wangu, zungumzeni kuhusu mimi, kuhusu kupanga mshambuliaji mmoja au washambuliaji wawili. Tukishinda 3-0 au 1-0, zungumzeni kuhusu rangi ya shati langu, kama natakiwa kwenda saloon kukata nywele au vinginevyo.”

“Zungumzeni vitu vingine lakini waacheni wachezaji wangu kwa sababu kila siku wanajitoa kwa asilimia 100 kwa ajili ya hii klabu, asanteni.”

Baada ya kuanza vyema kutetea taji la ASFC kwa kuifunga Majimaji FC mabao matano kwa sifuri jana Jumapili (Desemba 27), Simba SC itaendelea na mchakato wa kusaka alama tatu za Ligi Kuu kesho kutwa Jumatano (Desemba 30) kwa kuikaribisha Ihefu FC kutoka Mbeya.

Juma lijalo (Januari 06, 2021) Simba SC itakabiliwa na mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuikaribisha FC Platinum ya Zimbabwe, ambayo mchezo wa mkondo wa kwanza iliibuka na ushidni wa bao moja kwa sifuri.

Mngereza kuzikwa Jumatano Same
Majengo chakavu Zanzibar kufungwa