Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Sven Vandenbroeck, amewatoa hofu mashabiki na wanachama wa klabu hiyo ya Msimbazi kwa kusema shughuli itakayofanyika mwishoni mwa juma hili Uwanja wa Taifa dhidi ya Mwadui FC ni tofauti kabisa, na wataona mabadiliko makubwa.

Kocha Sven ametangaza uhakika wa mambo kuwaendea vyema katika mchezo ujao, baada ya kubanwa mbavu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting, uliomalizika kwa sare ya kufungana bao moja kwa moja, Uwanja wa Taifa Dar es salaam.

Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amesema kwa kusaidiana na benchi la ufundi la Simba SC, amefanya kazi kubwa ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo huo, ambao ulionyesha kuwakatisha tamaa mashabiki wa klabu hiyo kongwe nchini, hasa katika kipindi hiki cha matumaini ya kutetea ubingwa wao kwa mara ya tatu mfululizo.

Katika hatua nyingine kocha Sven, ameeleza kuwa, wachezaji wake walimuangusha katika mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Ruvu Shooting ambao walikuwa na malengo ya kuondoka na alama tatu.

“Baadhi ya wachezaji wangu waliniangusha kwa kucheza tofauti na vile ambavyo nilikuwa tunafanya mazoezini, tulifanya mazoezi ya mbinu na nguvu nyingi kwa kutambua tunakwenda kucheza dhidi ya timu yenye matumizi zaidi ya nguvu, lakini tulipofika uwanjani wachezaji wangu walionekana kuzidiwa mara kwa mara.

“Si mbaya tumedondosha alama mbili nyumbani na kupata moja na matatizo ambayo tumeyaona katika mchezo juu tutakwenda kuyafanyia kazi ingawa nafahamu kwa kukaa bila kuwa pamoja kwa zaidi ya miezi miwili lazima shida kama hizi zitokee,” amesema Sven.

“Tutabadilika na kuwa imara zaidi katika mechi ya Jumamosi,” aliongezea Sven.

Simba SC inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kumiliki alama 72,  baada ya kushuka dimbani mara 29 huku ikishinda michezo 23, kutoka sare michezo mitatu na kupoteza michezo mitatu.

Mpaka sasa mabingwa hao watetezi wameshafunga mabao 64 na kuruhusu kufungwa mabao 16.

Nyoni awaita Simba SC Jumamosi
Hitimana: Nipo tayari kumsajili Ngoma