Kocha mkuu wa kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania bara Simba SC, Sven Vandenbroeck ameliomba Shirikisho la soka Tanzania (TFF) liwape muda wa wiki mbili kujiandaa ligi ikirejea, baada ya kumalizika kwa mlipuko wa homa ya virusi vya Corona.

Kocha huyo kutoka Ubelgiji amesema, anafahamu wachezaji hawatakuwa na muunganiko sawa kwakua watakuwa hawajapata muda wa kufanya mazoezi ya pamoja kutokana na kusimama kwa ligi.

Michezo yote nchini imesimama kwa wiki ya tatu sasa kutokana na mlipuko wa homa ya virusi vya Corona ambayo inazidi kutikisa dunia kila kukicha.

“Nadhani tunahitaji kupewa wiki mbili za kujiandaa kufanya mazoezi ya pamoja baada ya hali kuwa shwari ili wachezaji wawe na muunganiko na ushindani uwe mkubwa kama ilivyokuwa mwanzoni,” alisema Sven.

Ligi Kuu imesimama huku Simba SC wakiwa wanaongoza kwa alama zao 71, wakifuatiwa na Azam FC alama 54 baada ya wote kucheza michezo 28, wakati vigogo Young Africans ni wa tatu kwa alama zao 51 za michezo 27 na Namungo wa nne wakiwa na alama 50 za michezo 28.

Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa alama zake 15 za michezo 29, nyuma ya Mbao FC wenye alama 22 za michezo 28, Alliance FC alama 29, michezo 29, Mbeya City alama 30 michezo 29 na Ndanda FC alama 31 michezo 29.

Reliants Lusajo: Elimu yangu ina msaada mkubwa Namungo FC
Gwajima aiomba radhi Congo kuhusu chanjo ya Corona

Comments

comments