Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema jumla ya taasisi za umma 455 zimeunganishwa na zinatumia mfumo mpya wa taarifa za kiutumishi na mishahara ili kupunguza muda wa kuchakata malipo ya mishahara kutoka siku 14 hadi siku moja pamoja na kuwa na taarifa sahihi za watumishi wanaotarajia kustaafu.

Majaliwa, ameyasema hii leo Novemba 11, 2022 jijini Dodoma wakati akizungumzia utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa umma,na kusema Serikali imeendelea kuboresha, kuimarisha na kuweka mifumo imara ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utendaji kazi wa watumishi wa umma na taasisi za umma ili kuhakikisha kuwa mifumo iliyopo na inayojengwa inasaidia kuharakisha utendaji kazi.

Amesema mfumo huo mpya ambao ulianza kutumika rasmi Mei 2021, umeunganishwa na mfumo wa PSSSF kwa ajili ya kubadilishana taarifa za michango ya watumishi na nyaraka za hitimisho la ajira, mfumo wa mikopo ya elimu ya juu (HESLB), kwa ajili ya kubadilishana taarifa za mikopo ya elimu ya juu kwa watumishi, mfumo wa ajira portal kwa ajili ya kubadilishana taarifa za waajiriwa wapya na mfumo wa NIDA kwa ajili ya kubadilishana taarifa za utambulisho wa Taifa wa watumishi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Aidha ameitaja mifumo mingine kuwa ni ile iliyojengwa kwa lengo la kukabiliana na changamoto za upimaji wa utendaji kazi wa watumishi na mikataba ya utendaji kazi ya taasisi kuwa ni Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma (PEPMIS) na Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Taasisi za Umma (PIPMIS).

Amesema, hatua ya mifumo hiyo kuwa ya kielektroniki itaondoa muhali, hisia za kupendeleana au kuoneana katika usimamizi wa utendaji kazi na itahamasisha uwajibikaji wa hiari wa watumishi wa umma itakayosaidia utoaji huduma bora na kwa wakati kwa umma wa Watanzania.

Rais mstaafu aishitaki Kamati ya Bunge
Uchumi wazidi kudorora, bajeti mpya kutangazwa